Wajasiriamali wakumbushwa ubora viwango

14Jan 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wajasiriamali wakumbushwa ubora viwango

WAJASIRIAMALI nchini wameshauriwa kutumia fursa iliyotolewa na serikali kupitia programu mbalimbali ili wathibitishe bidhaa wanazozalisha kwa lengo la kuziongezea thamani, kwa kuwa na viwango vya ubora vinavyotakiwa sokoni.

Akizungumza baada ya kukabidhibiwa cheti cha ubora kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Meneja Mkuu wa Mbalawala Women Organisation iliyopo Mbinga mkoani Ruvuma ambayo ni wazalishaji wa mkaa mbadala, Leah Kayombo, alisema wajasiriamali wanapaswa kutumia utaalamu kuthibitisha bidhaa zao ili kuleta ushindi sokoni.

“Bidhaa yetu ya mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe imethibitishwa na tumepatiwa cheti cha ubora, imetupa nguvu ya kuendelea kuzalisha kwa kuwa mkaa huu  ambao ni mwokozi wa mazingira utapunguza ukataji
miti kwa  kuchoma mkaa na kuni,” alisema Kayombo.

Alisema walishawishika kuanza uzalishaji wa mkaa huu kutokana na athari za kimazingira ambazo zinaendelea kutokea ulimwenguni, hivyo kwa kuunga mkono juhudi za serikali za kutunza mazingira kama wajasiriamali wameanza kuzalisha mbadala utakaosaidia kutunza mazingira.

Alishukuru TBS na serikali kwa ujumla kwa kutoa fursa ya mafunzo juu ya ubora wa bidhaa na utoaji wa vyeti vya ubora pasipo na gharama yoyote, hivyo anawahamasisha wajasiriamali wengine nchini kutumia fursa hii ili wapate uthibitisho wa bidhaa zao kabla ya kuingia sokoni.

Kayombo aliishukuru kampuni ya uchimbaji makaa ya mawe ya TANCOAL kwa kuendelea kuwafadhili, Serikali ya Mkoa wa Ruvuma kwa kuwawezesha mpaka kufikia kupata cheti hicho ambacho kitawafanya kufanya biashara kwa uhuru na pia kuweza kufungua mipaka katika usambazaji.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TANCOAL, James Shedd, ambao ni wafadhili wakuu wa Mbalawala Women Organisation, alisema hatua waliyofikia ni nzuri na wamezidi kupata moyo wa kuendelea kuwafadhili katika kufanya uzalishaji wa mkaa wenye tija ikiwa ni sehemu ya kampuni kurudisha katika jamii.