Wajasiriamali waonywa kujitwika majukumu yote

18Mar 2019
Nebart Msokwa
MBOZI
Nipashe
Wajasiriamali waonywa kujitwika majukumu yote

ASILIMIA 80 ya biashara zinazoanzishwa sehemu mbalimbali haziendelei kutokana na wamiliki wake kutozingatia misingi ya uendeshaji, ikiwamo kutekeleza majukumu yote wenyewe badala yake kuunda timu ya utatu kushughulikia maeneo muhimu.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo (kulia), akizungumza na baadhi ya wajasiriamali wa wilaya hiyo walionufaika na mradi wa uwezeshaji wa biashara unaotekelezwa na Shirika la Heifer International kwa kushirikiana na Taasisi ya Sirolli. PICHA: NEBART MSOKWA

Aidha, timu hiyo ya utatu huundwa na wasimamizi wa uzalishaji, watafuta masoko na wasimamizi wa fedha na kwamba ndicho wanachowafundisha wajasiriamali sasa.

Hayo yalisemwa juzi wilayani Mbozi mkoani Songwe na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sirolli kutoka nchini Marekani, Dk. Ernest Sirolli, kwenye Mradi wa Uwezeshaji wa Biashara (Sirolli) kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Mbozi mkoani humo.

Mradi huo unafadhiliwa na Shirika la Heifer International na kutekelezwa na shirika hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya Sirolli, unaotekeleza na taasisi hiyo kwa kushirikiana na Shirika la Heifer International ambalo pia ndilo mtekelezaji.

Alisema ili biashara yoyote iweze kufanikiwa ni lazima iendeshwe kwa kuunda timu ya utatu yaani kuwapo na wasimamizi wa uzalishaji, watafuta masoko na wasimamizi wa fedha na kwamba ndicho wanachowafundisha wajasiriamali wa Mbozi.

Aliongeza kuwa  mradi huo ni wa majaribio na unafanyika kwa muda wa miaka miwili kuanzia Oktoba 2017 na unatarajiwa kufikia ukomo Juni 2019 na kwamba unafadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Heifer International.

“Tunatoa ushauri bure na kwa usiri kwa mtu yeyote anayehitaji, mwenye wazo la biashara au anataka kukuza na kuendesha biashara, ni muhimu  mjasiriamali kujua mahali soko lilipo, ubora wa bidhaa zinazohitajika na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha,” alisema Dk. Sirolli.

Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Heifer International Tanzania, Rose Marando, alisema mradi huo ni wa vikundi na unalenga kuimarisha biashara za vikundi hivyo kwa kutoa elimu juu ya uendeshaji wa biashara hizo.

Aliwaeleza wajasiriamali kuwa Heifer International iliamua kufadhili mradi huo baada ya kubaini kuwa wajasiriamali wengi wanakabiliwa na changamoto nyingi kama kukosa saikolojia ya biashara kwa kutojua taratibu za utunzaji wa kumbukumbu na kutenganisha mtaji na faida.

Alisema wakati mwingine wajasiriamali wanajikuta kila kitu kinakuwa kigumu kwao kwa kujikuta wakati mwingine wanachukua mtaji na kuingiza kwenye matumizi ya nyumbani.

“Mara nyingi tumeona mjasiriamali huyo anazalisha bidhaa, anatafuta masoko mwenyewe na anatunza fedha mwenyewe hali ambayo inafika wakati vyote vinakuwa vigumu kwake, sasa tumekuja na kitu kinaitwa ‘utatu wa biashara’ au business psychology (saikolojia ya biashara au Trinity of management”), alisema Marando.

Alisema kikundi kinaweza kikawa cha marafiki ama wanafamilia ili mradi wanaelewana na kila mtu anatakiwa kufanya kitu anachokifahamu na kwamba mradi huo utasaidia kuondoa fikra za jamii kuwa fedha zao zinachukuliwa na ‘chuma ulete.’

Ofisa Uhusiano wa Heifer International Tanzania, Mercy Nyanda, aliwataka wafanyabiashara wa Wilaya ya Mbozi kuutumia vizuri mradi huo kwa maelezo  kuwa utawasaidia kuimarisha biashara zao kwa kuhakikisha zinakuwa endelevu.

Alisema mradi huo una madaktari wa biashara ambao watawapatia elimu ya namna ya kuendesha biashara zao kwa faida na kutunza kumbukumbu za biashara hizo.

Habari Kubwa