Wajasiriamali wapewa fursa makao makuu

20Dec 2016
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Wajasiriamali wapewa fursa makao makuu

MEYA wa Manispaa ya Dodoma, Jaffar Mwanyemba, amewataka wajasiriamali wa mkoani hapo kutumia fursa ya ujio wa makao makuu ya serikali kujiongezea kipato.

Akifungua mafunzo ya wajasiriamali iliyoandaliwa na Mbunge wa Jimbo la Dodoma, Anthony Mavunde, kwa kushirikiana na kampuni ya Hi-Tech International ya jijini Dar es Salaam, Mwanyemba alisema ujio huo utaleta watu wengi kutoka nje ya mkoa huo na watawekeza.

“Wajasiriamali tumieni fursa hii kabla watu hawa hawajafika kwa kutafuta namna ya kujiongezea kipato, Dodoma inakuwa makao makuu ya nchi tusizubae watakuja watu kutoka Mwanza, Arusha, sababu ya sisi kutokutumia fursa tutajikuta,” alisema.

Mwanyemba alisema watu wa Dodoma ndio wamekuwa wakiajiriwa kwa shughuli mbalimbali hivyo wasikubali wawe watazamaji bali makao makuu yawanufaishe.

Aliwaasa kuwa na nidhamu na kuiheshimu mikopo wanapokopa kwenye taasisi mbalimbali za fedha na kuacha kutumia kwenye starehe.

“Pia biashara zenu mfanye kwenye maeneo ambayo ni rasmi na muache kung’ang’ania kufanya barabarani kama wanavyofanya wamachinga,” alisema.

Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Vijana, alisema amejipanga kuifanya Dodoma inakuwa ya viwanda.

“Nitahakikisha nawasaidia wajasiriamali kwa kuwatafutia fursa mbalimbali zilizopo nchini ili waweze kufikisha malengo yao waliyojiwekea, ikiwa ni pamoja na kuanzisha viwanda vidogo vidogo,”alisema Mavunde

Naye mkurugenzi wa kampuni ya Hi-Tech International, Paul Mashauri, aliwataka wajasiriamali kuwa na uthubutu na hamu ya mafanikio kwa kuwekeza katika biashara mbalimbali.

Habari Kubwa