Wajasiriamali wapewa mtego bidhaa za viwango

20Mar 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Wajasiriamali wapewa mtego bidhaa za viwango

MTANDAO wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata), umewataka wajasiriamali kutengeneza bidhaa bora na zenye viwango ambazo zitauzwa bei nafuu ili kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Kadhalika wametakiwa kutumia nyenzo na maarifa mbalimbali wanayopata katika mafunzo ya usindikaji wa mazao ya vyakula na mifugo.

Mratibu wa Mviwata mkoani hapa, Richard Masandika, aliyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya usindikaji wa mazao ya vyakula na mifugo kwa washiriki 23 kutoka wilayani Karatu.

"Nawataka mtumie vizuri mafunzo haya mliyoyapata, msiishie njiani, tumieni weledi kutengeneza bidhaa bora zenye viwango
ambazo zitapata masoko kwa urahisi ndani na nje ya nchi hii," alisema.

Mapema Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo nchini, (SIDO), Mkoa wa Arusha, Nina Nchimbi, aliwasisitiza wajasiriamali wote kuwa na vitambulisho vya ujasiriamali ambavyo vinatolewa nchi nzima katika kata husika ili warasimishwe rasmi katika biashara na bidhaa zao.

Aliwataka wajasiriamali wote nchini kuhakikisha wanaanzisha viwanda vidogo vidogo na wengine kuajiriwa katika viwanda hivyo lengo likiwa ni kujiongezea kipato na uchumi wa taifa kwa ujumla ikiwamo kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.

"Nyie wajasiriamali, hakikisheni mafunzo haya mliyoyapata mnatengeneza na kusindika bidhaa zote mlizofundishwa, nawapongeza kwa jitihada mlizoonyesha kwa siku chache mlizokaa hapa mmejifunza zaidi ya kusindika bidhaa 20, hongereni sana, myafanyie kazi kwa vitendo," aliwasihi.

Mratibu wa mafunzo hayo kutoka SIDO, mkoani hapa, Bahati Mkopi, aliwataka wajasiriamali wote wenye nia ya kuwa na ujuzi wa kusindika mazao ya vyakula na mifugo wasisite kufika kwenye shirika hilo ili kupatiwa mafunzo na nyenzo mbalimbali.

Habari Kubwa