Wakamatwa kwa tuhuma ya biashara ya ukahaba

19Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Wakamatwa kwa tuhuma ya biashara ya ukahaba

WANAWAKE 20 wamekamatwa Zanzibar wakituhumiwa kujihusisha na biashara ya ukahaba na mapenzi ya jinsia moja.

Operesheni ya kuwasaka watu wanaofanya biashara ya ukahaba na kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja ilifanyika juzi na kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud, chini ya mpango wake wa kupambana na vitendo hivyo pamoja na dawa za kulevya.

“Operesheni hii imefanyika kutokana na kuwapo taarifa za vitendo vya ukahaba katika maeneo tofauti pamoja na serikali kupiga marufuku,” alisema Mahmoud.

Alilitaka Baraza la Manispaa Zanzibar kuifutia leseni nyumba moja ya kulaza wageni visiwani hapa kwa madai ya kukiuka mashariti ya uendeshaji wa biashara hiyo.

Alisema watu hao walikamatwa wakiwa katika nyumba hiyo ya kulala wageni na katika baa moja ambayo tayari imefutiwa leseni ya kuendesha biashara.

Operesheni hiyo ilifanyika majira ya kati ya saa 4:00 na 6:00 usiku, akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Marina Joel Thomas, ambaye aliwataka wananchi kutoa ushirikiano ikiwemo kuwafichua watu wanafanya vitendo hivyo.

Alisema katika wilaya yake vitendo vya ukahaba vimekuwa vikiongezeka ndiyo maana serikali ya mkoa imeamua kupiga vita vitendo hivyo ili kulinda mila na utamaduni wa Zanzibar.

Habari Kubwa