Wakulima 816 wawashangaa viongozi wa wilaya, mkoa

15Mar 2017
Godfrey Mushi
SAME
Nipashe
Wakulima 816 wawashangaa viongozi wa wilaya, mkoa

WAKULIMA zaidi ya 816 wa kata ya Ndungu, wilaya ya Same wameeleza kushangazwa na ukimya wa viongozi wa serikali wilayani humo na wa mkoa wa Kilimanjaro kuhusu changamoto zinazoukabili mrefeji wa umwagiliaji maji wa Fidia uliokwama kufanyakazi kutokana na itikadi za kisiasa.

Mfereji huo ulijengwa na serikali ya kikoloni ya Waingereza kati ya mwaka wa 1958 na 1960 kwa lengo la kumwagilia mazao ya aina mbalimbali.

Juzi Katibu wa chama cha wakulima wenye mashamba wanaotumia mfereji wa Fidia (Sorovea), Ombeni Juma, aliyasema hayo juzi wakati Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), Naghwenjwa Kaboyoka, alitembelea mrefeji huo na kukutana na wakulima.

“Mheshimiwa Mbunge tangu tulipoamua wenyewe wakulima tusiozidi 28 kuufufua mfereji huu kwa kuuchimba kilomita 6.6 kwa mkono, mpaka sasa hakuna kiongozi yeyote wa serikali ngazi ya wilaya na mkoa aliyekuja kututazama. Tunakuomba umlete Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba aje atusikilize kero yetu,” alisema Ombeni.

Awali, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Ndungu, Paulo Gilbert, alimweleza Kaboyoka kwamba kwa miaka mingi mfereji huo haukufufuliwa, hadi yeye alipowahamasisha wananchi ambao walichanga zaidi ya Sh. milioni nne kwa ajili ya kujenga kivuko cha kuvushia maji eneo la Nambanne.

“Inashangaza badala watu watumie fursa hiyo kukabiliana na upungufu wa chakula, wafanyakazi ya kulima kama Rais anavyosisitiza, wao wanaingiza itikadi za kisiasa.

Hivi sasa tunahitaji fedha za kuujenga mfereji huo kwa saruji lakini hakuna hata kiongozi anayefika kuuona, wakija wanapigwa siasa na kuondoka,” alisema.

Hata hivyo, pamoja na changamoto zilizopo, wakulima wa Ndungu wamefanikiwa kulima mahindi hekta 250, kati ya 319 zilizopo katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa Kaboyoka, mwaka 1983 serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ilianza maandalizi ya ujenzi wa mfereji wa Bonde la Mkomazi linalojumuisha eneo la Ndungu, chini ya mradi uliojulikana kama Ndungu Development Project na wakati huo wakulima ambao hawakupata mashamba kwenye mfereji wa Ndungu waliendelea kutumia mfereji wa Fidia.

Mfereji huo ulikamilika mwaka 1990 na ulikuwa na uwezo wa kuhudumia eneo la hekta 680 ambazo zingeweza kulimwa mara mbili kwa mwaka na wakulima 13,000 wa vijiji vya Ndungu, Misufini na Kalemawe.

Mkuu wa Wilaya ya Same Rosemary Sitaki, alipotafutwa kwa njia ya simu kujibu malalamiko ya wananchi hao simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa.

Habari Kubwa