Wakulima kahawa watangaziwa neema

14Jun 2018
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Wakulima kahawa watangaziwa neema

CHAMA cha Msingi cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Lyamungo (Amcos), Wilaya ya Hai kimetangaza ‘neema’ kwa wazalishaji wadogo wa kahawa mkoani Kilimanjaro baada ya kutenga Sh. milioni 120 za ununuzi wa kilogramu 40,000 za kahawa msimu huu.

Ununuzi huo utahusu kahawa iliyovunwa katika msimu wa mwaka 2018/2019 ambao serikali ilitangaza uamuzi mgumu wa kuzuia mawakala kununua zao hilo moja kwa moja kutoka kwa wakulima.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Kilimo na  Masoko wa Lyamungo Amcos,  Gabriel Ulomi alitangaza hayo juzi wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho ulioketi kwa ajili ya kupitisha bajeti ya mapato na matumizi ya mwaka 2018/2019.

“Vyama vya msingi sasa vinakwenda kukusanya kahawa vyenyewe na hakutakuwa na mnunuzi yeyote binafsi vijijini hii itasaidia kuinua uchumi wa vyama vyetu, lakini pia wakulima wanaofanya shughuli za kilimo cha kahawa wataweza kunufaika zaidi,” alisema Ulomi.

Ulomi alisema kwa msimu huu, chama hicho kitaanza kununua kahawa ya wakulima kwa Sh. 2,000 kwa kila kilogramu moja ya kahawa ghafi, kabla ya kwenda mnadani.

Alisema msimu uliopita wa mwaka 2017/2018 waliuza kahawa mnadani  kwa Sh. 4,200 kwa kilogramu moja na kwamba msimu huu wanatarajia kuuza kahawa yao kwa Sh. 5,000 kwa kilogramu moja kwa bei ya sokoni.

Aidha, chama hicho kinakusudia kutumia Sh. milioni 120 kwa ajili ya kuendeshea miradi mbalimbali ya chama hicho msimu 2018/2019 ukiwamo mradi wa zao la kahawa, alizeti, mradi wa shamba na duka.

Miradi mingine ni mashine ya kusaga na kukoboa nafaka na ufyatuaji tofali za ujenzi, ukodishaji viti na miradi ya kilimo cha mboga.

Pamoja na mambo mengine, Ulomi alisema msimu uliopita chama chake kimefanikiwa kutumia faida yake kusaidia miradi mbalimbali ya kijamii ikiwamo ujenzi wa viwanja vya michezo na ujenzi vyumba 13 vya madarasa katika Shule ya Sekondari Lyasikika.

Alisema pia walitumia zaidi ya shilingi milioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa vyoo katika Shule ya Msingi Ari na ukarabati wa barabara yenye urefu wa kilometa 12 hadi 18 ikiwamo ujenzi wa vivuko vya barabarana kuchangia Shilingi 10,000 kwa ajili ya bima ya afya.

 

 

 

Habari Kubwa