Wakulima korosho wachangamkia msimu

22Oct 2019
Hamisi Nasiri
Newala
Nipashe
Wakulima korosho wachangamkia msimu

ZAIDI ya tani 200 za korosho zimeshakusanywa kwenye maghala ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Newala pamoja na Tandahimba Cooperative Union (TANECU) mkoani Mtwara kwa msimu wa mwaka 2019/2020.

Hayo yalisemwa wilayani Newala na Mkuu wa Wilayani ya Newala, Aziza Mangosongo, baada ya kutembelea maghala ya Tanecu, Agrofocus na Splenders Control Ltd, na kusema kuwa baada ya msimu kufunguliwa, angefanya ziara hiyo ili kuona hali ya maghala na jinsi yalivyoanza kufanya makusanyo ya korosho kwa msimu huu.

Alisema hali ya maghala inaridhisha na kuwa matumaini yake ni kuwa mwitikio wa wakulima umekuwa chanya zaidi katika kukusanya korosho hizo.

"Kwenye Amcos nilizotembelea nimekuta tayari zipo tani 400 ambazo zinatarajia kufika kwenye vyama muda si mrefu mambo yote yako vizuri na tumejipanga kwenye magunia na kuhakikisha usalama wa wakulima wakati wa kuleta korosho zenye ubora kwa wakati,” alisema Mangasongo.

Makamu Mwenyekiti wa TANECU, Shaibu Njauka, alisema kwa Wilaya ya Tandahimba kwenye ghala la Tandahimba limeshapokea kiasi cha tani 76,565 za korosho kutoka kwa baadhi ya AMCOS na bado zoezi linaendelea kwa kasi kubwa.

"Makusanyo yameanza kwa kasi kubwa na upo uwezekano wa kupata mzigo mkubwa ndani ya wiki, hivyo msimu umeshafunguliwa… korosho zipelekwe Amcos zikiwa kwenye madaraja ili kuziwahisha sokoni, maghala yako wazi korosho za msimu uliopita hazipo sasa tunakusanya korosho mpya kwa Newala na Tandahimba," alisema Njauka.

Mashua Said, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Enganero Kata ya Mkunya wilayani Newala, alisema ndani ya siku tatu amefanikiwa kukusanya zaidi ya tani 60, hali ambayo imempa hofu kutokana na wingi huo wa korosho.

Habari Kubwa