Wakulima kukatwa kodi kwa kuuza mahindi

23May 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Wakulima kukatwa kodi kwa kuuza mahindi

SERIKALI imetoa ufafanuzi kuhusu wakulima au kikundi katika Wilaya ya Moshi kinachotaka kuuza mahindi katika Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kwenye ghala lake lililoko Arusha kuwa watakatwa kodi ya zuio ya asilimia mbili.

Kwa mujibu wa notisi iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Kastori Msigala, mahindi yanayopaswa kuuzwa ni yale yaliyovunwa katika msimu wa mwaka 2017/18.

Katika notisi hiyo iliyotolewa na Msigala, serikali kupitia NFRA, hivi sasa inanunua mahindi hayo katika Ofisi ya Kanda ya Mikoa ya Kaskazini iliyoko mkoani Arusha.

"Bei elekezi iliyopitishwa ghalani ni Sh. 490 kwa kilo moja. Aidha, mkulima au kikundi kitakatwa kodi ya zuio asilimia mbili  na mahindi yatafanyiwa ukaguzi wa ubora kabla ya kuidhinishwa kupokewa," alisema Msigala.

Aidha, mkurugenzi huyo alisisitiza kuwa malipo ya mahindi hayo yatakayopelekwa kuuzwa ghalani, yatafanyika baada ya saa 48.

Wakati halmashauri hiyo ikitangaza kuwapo kwa suala hilo, katika maeneo ya vijiji vilivyoko ukanda wa milimani hasa Old Moshi, bei ya mahindi kwa gunia moja la kilo 100 ni Sh. 75,000.

Alipoulizwa Diwani wa Old Moshi Mashariki, Andrew Ringo, kuhusu uuzaji wa mahindi katika eneo hilo, alisema ni kweli gunia moja la mahindi limefikia bei hiyo sokoni.

Masoko ya mazao kama Kwa Sadala, Wilaya ya Hai na Sanya Juu katika Wilaya ya Siha, bei ya mahindi kwa gunia moja imefikia Sh. 80,000.