Wakulima mananasi wapewa teknolojia mpya ya uzalishaji nje ya msimu

16Sep 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Wakulima mananasi wapewa teknolojia mpya ya uzalishaji nje ya msimu

WAKULIMA wa zao la nanasi Tarafa ya Mkuyuni, Wilaya ya Morogoro, wamepewa teknolojia mpya ya kuzalisha zao hilo nje ya msimu wa matunda ili kufanya kilimo biashara kwa kuuza katika kampuni za kutengeneza juisi na vinywaji baridi.

Teknolojia hiyo ya asili inamfanya mkulima kutumia vipande vya ndizi kuwekwa kwenye tawi la nanasi inayosaidia kuwahisha ua la nanasi kuzaa kabla ya msimu wa matunda mengine.

Akizungumzia Teknolojia hiyo mpya,Bwana shamba wa tarafa ya Mkuyuni kupitia mradi huo unafahamika kama Mali mbichi,Asela Kavishe,alisema kuwa teknolojia hiyo inamfanya mkulima wa nanasi kuwa na uhakika wa soko lake.

Alisema teknolojia hiyo inamfanya mkulima kuzalisha nanasi kipindi ambacho hakuna matunda mengine kama maembe, machungwa na mapasheni, katika masoko na kumwezesha mkulima kujipangia bei.

Dk. Elias Mgembe, kutoka Idara ya Sayansi ya mimea na mazao ya bustani ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua), alisema teknolojia hiyo imeanza kutumiwa na wakulima wachache katika eneo hilo na imeonyesha mafanikio.

Dk. Mgembe ambaye ni mtafiti mwandamizi, alisema wamebuni teknolojia hiyo kuwasaidia wakulima wa nanasi ambao wamekuwa wakipata hasara kutokana na matunda wanayozalisha kukutana na matunda mengine katika msimu mmoja na kushindwa kufanya kilimo biashara.

Mmoja wa wakulima hao, aliyeanza kuzalisha nanasi kwa kutumia teknolojia hiyo, Mohamed Mitapwa, alisema awali alikuwa akilima hekari moja na kuvuna mananasi kati ya 200 katika msimu wa matunda, lakini baada ya kutumia teknojia hiyo mpya, anavuna mananasi mpaka 800 kwa hekari moja na kipindi ambacho sio msimu wa matunda.

Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Matunda katika tarafa ya Mkuyuni, Burhan Mgambi, alisema uzalishaji wa nanasi kwa kila msimu umekuwa ukifikia wastani wa tani 1000, lakini zimekuwa zikikosa soko kutokana na kipindi hicho matunda mengine kama maembe kuwa kwenye soko.

Alisema kutokana na mwingiliano huo, katika msimu mmoja umesababisha wakulima wa nanasi katika tarafa hiyo kukosa soko na hivyo kujikuta matunda hayo yakiharibika au kuuza kwa bei ya hasara, huku wakiwa wanadaiwa mikopo na taasisi za fedha.

Mratibu wa mradi wa Malimbichi kutoka Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (Mviwata), Ernest Likoko,,alisema wameshazungumza na kampuni kubwa ya uzalishaji wa juisi kuwa wapo tayari kununua mananasi ya wakulima hao nje ya msimu wa matunda.

Habari Kubwa