Wakulima Mbarali kusajiliwa kuondolewa usumbufu

29May 2020
Grace Mwakalinga
Mbarali
Nipashe
Wakulima Mbarali kusajiliwa kuondolewa usumbufu

SERIKALI wilayani Mbarali katika Mkoa wa Mbeya, imetakiwa kuwasajili na kuwatambua wakulima wote hasa wa mpunga ili kuwaondolea usumbufu wa kukamatwa wanaposafirisha mazao yao kutoka shambani wakidhaniwa kuwa ni wafanyabiashara wanaokwepa ushuru wa mazao.

Hayo yalibainishwa jana na Katibu wa Jukwaa la Wakulima na Wafugaji, Christopher Uhagile, wakati akizungumza na Nipashe na kusema kuwa sheria ndogo ya ushuru wa mazao inakiukwa kwa kuwalazimisha wakulima wanaosafirisha mazao yao kutoka mashambani kulipa ushuru kwa vile sheria hiyo inaelekeza anayepaswa kulipa ushuru huo ni mnunuzi wa mazao na sio mkulima.

Alisema ili kuondoa adha wanayokabiliwa nayo wakulima wanapotoa mazao yao shambani na kupeleka nyumbani, jukwaa hawana ubishi kwamba lazima ushuru ulipwe, lakini tatizo ni nani anatakiwa kulipa ushuru huo.

“Katika kutatua shida ya wakulima wa mpunga kutozwa faini, jukwaa nimeomba serikali ya wilaya kupitia watendaji wa vijiji kuwatambua wakulima wote ili iwe rahisi kuwatoza wafanyabiashara wanaostahili,” alisema Uhangile.

Aliongeza kuwa serikali haina budi kuwatambua wanunuzi wa mazao vijijini na kupiga marufuku ununuzi wa mazao yaliyo mashambani kwa madai kuwa kitendo hicho kinaikosesha serikali mapato kutokana na wanunuzi wa mazao yaliyo mashambani kujifanya ni wakulima.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakulima na Wafugaji, Matagili Mbigili, aliwataka wakulima wilayani Mbarali kuheshimu maeneo ambayo ni mapito ya mifugo ili kuepusha migogoro na ugomvi baina yao na wafugaji.

Alisema hata hivyo, serikali iliruhusu usafirishaji wa mazao yasiyozidi tani moja bila kulipiwa ushuru, fursa ambayo sasa imeanza kutumiwa vibaya na wafanyabiashara kukwepa kulipa ushuru wa mazao, lakini msamaha huo unawakandamiza wakulima wanaopata mavuno mengi yanayozidi tani moja, wanapoyasafirisha kutoka mashambani.

Habari Kubwa