Wakulima mpunga wanufaika na soko la Kenya

30Jul 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Wakulima mpunga wanufaika na soko la Kenya

​​​​​​​MAKUBALIANO ya kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya serikali ya Tanzania na Kenya yameanza kuleta neema kwa wakulima wa nafaka mkoani Mbeya baada ya shehena ya mchele unaozalishwa mkoani hapa kuanza kusafirishwa kwenda Kenya.

Hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan akiongozana na maofisa mbalimbali wa serikali, walifanya ziara nchini Kenya na kufanya kikao na Rais Uhuru Kenyata wa nchi hiyo ambapo pamoja na mambo mengine, walikubaliana kuondoa vikwazo vya kibiashara baina ya mataifa hayo.

Juzi, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Juma Homera na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk. Tulia Ackson, ilifanya ziara katika kiwanda cha kukoboa mpunga cha Kampuni ya Raphael Group Ltd, Uyole jijini Mbeya.

Katika ziara hiyo, kamati hiyo ilishuhudia shehena kubwa ya mchele ukiwa unapakiwa kwenye malori tayari kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya huku mmiliki wa kiwanda hicho, Raphael Ndelwa, akisema bado kuna mahitaji makubwa ya mchele nchini humo.

Ndelwa alisema tangu marais hao walipokubaliana kuondoa vikwazo, kumekuwa na mahitaji makubwa ya mazao ya nafaka nchini Kenya hali ambayo alisema itasaidia mazao ya wakulima kupata soko la uhakika nchini humo.

“Hivi mnavyoona hili lori limeshajaa na linaondoka muda si mrefu kupeleka mchele huu Nairobi. Lakini kuna wateja wengine wanatuma magari yao yanakuja kubeba mchele hapa. Tunao  mchele wa kutosha kwa ajili ya soko hilo na bado wakulima wanaendelea kutuletea,” alisema Ndelwa.

Alisema mbali na mpunga pia amekuwa akinunua mazao mbalimbali kutoka kwa wakulima yakiwamo maharage, karanga na alizeti kisha kuyauza baada ya kuyaongezea thamani.

Ndelwa alisema matatizo yanayokikabili kiwanda chake ni ukosefu wa maeneo ya kutosha kwa ajili ya kutunza mpunga hali iliyosababisha waurundike nje lakini akasema ni hatari endapo mvua itanyesha muda wowote.

Alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, wameomba mkopo wa zaidi ya Sh. bilioni tatu kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa ajili ya kujenga maghala ya kuhifadhia mazao hayo na kwamba eneo tayali wanalo.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Homera, aliridhishwa na uwekezaji wa kiwanda hicho ambacho kinamilikiwa na mwekezaji mzawa kutokana na kuwa na mitambo ya kisasa ya kukoboa mpunga na kuuchambua katika madaraja mbalimbali.

Alisema kutokana na kuridhishwa na uwekezaji wa kiwanda hicho, watahakikisha wanamsaidia kuweka msukumo kwa Benki ya TADB ili apatiwe mkopo alioomba na kisha kuendeleza uwekezaji anaouhitaji.

Alisema mwekezaji huyo ni miongoni mwa wawekezaji wachache wenye mwelekeo mzuri kutokana na kuwa na ushirikiano mzuri na wakulima wadogo kutoka katika mikoa mbalimbali ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.

Naye Dk. Tulia ambaye ni Naibu Spika, alisema kiwanda hicho mbali na kuchangia kukua kwa pato la taifa pia kimesaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.

Alisema mwekezaji wa kiwanda hicho ana elimu ya darasa la saba, lakini ameajiri wasomi wenye shahada mbalimbali zaidi ya 40 na vibarua wengine zaidi ya 200 wanaofanya kazi kwenye idara mbalimbali za kiwanda.

Habari Kubwa