Wakulima mwani wapatiwa vipande vya kamba 700,000

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wakulima mwani wapatiwa vipande vya kamba 700,000

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dk. Rashid Tamatamah, amekabidhi vipande vya kamba za manila 700,000 kwa wakulima wa mwani katika Kijiji cha Songosongo, wilayani Kilwa, Mkoa wa Lindi.

wakulima wa mwani.

Akizungumza na wananchi wa Songosongo juzi, Dk. Tamatamah alisema serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Sekta ya Uvuvi) imetoa kamba hizo ili kuwawezesha wakulima wa mwani kwani kamba ilikuwa ni moja ya changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo.

 

Kamba hizi za manila (ambazo kila moja ina urefu wa mita 10) katika kilimo cha mwani, hufungwa katika vigingi na hutumika kwa ajili ya kuoteshea mwani, ambapo mwani hufungwa katika kamba hizo zinazosaidia pia mwani kutochukuliwa na maji ya bahari pale panapokuwapo na wimbi.

 

Dk. Tamatamah alisema duniani kote kwa sasa mwani unalimwa kibiashara, hivyo mwani ni moja ya zao linalopewa kipaumbele katika wizara. Katika kilimo cha mwani wakulima wanakutana na changamoto mbalimbali zikiwamo za ukosefu wa mitaji na masoko.

 

“Wizara kupitia sekta ya uvuvi imeanza kutoa kamba ambazo ni moja ya pembejeo muhimu kwa wakulima wa mwani ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wakulima hao kwa kuwapunguzia sehemu ya gharama za uzalishaji ili baadaye waweze kusimama wenyewe,” alisema Dk. Tamatamah.

 

Pia, alisema kama wakulima watalima vizuri katika kamba moja ya mita kumi katika bamvua nne (miezi miwili), wanaweza kupata kati ya kilo 8-10, na kamba hizo walizopewa zinaweza kutumika kwa mwaka mzima. Lengo la wizara ni kusambaza kamba hizi kwa wakulima wa mwani maeneo yote Tanzania Bara.

 

Kwa mujibu wa Dk. Tamatamah, ipo changamoto ya soko la mwani hasa kwenye bei kwani kwa sasa asilimia 90 ya mwani inauzwa nje ikiwa ghafi na ni asilimia 10 tu ndio inayotumika hapa nchini.

 

“Hivyo wizara kwa sasa inawahamasisha wakulima kujiunga katika vikundi na kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili waweze kukopesheka na waweze kuanzisha viwanda vidogo vya kuchakata mwani ili kuuongezea thamani. Hii itasaidia kupunguza kiasi cha asilimia ya mwani inayokwenda nje ya nchi ikiwa ghafi na kusaidia kuongeza ajira,” alisema.

 

Aidha, Tamatamah alisema zao la mwani linazo faida kubwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kipato katika jamii za maeneo ya pwani hasa kwa kinamama, inaondoa umaskini lakini pia linaingiza fedha za kigeni.

 

Naye mkulima wa mwani, Mbimbisa Omary, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kuwaletea vitendea kazi kwa ajili ya kilimo cha mwani.

Mbimbisa alisema kilimo cha mwani kinawasaidia mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasomesha watoto, kununua chakula pamoja na ujenzi wa nyumba.

 

Jaka Farahani, mkulima wa mwani, alisema changamoto ya masoko inawasumbua sana hasa pale wanunuzi wanaowategemea wasiponunua, hivyo aliiomba wizara kuwasaidia kutatua changamoto hiyo.

Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji (WMUV), Dk. Nazael Madalla, alisema wizara kupitia idara yake inaendelea kuhamasisha kampuni kuendelea kuchukua leseni kwa ajili ya kununua mwani na mpaka sasa zipo kampuni 7. Lengo la kuwa na kampuni nyingi ni kuongeza ushindani hivyo kampuni zinahamasishwa kujisajili ili zitambulike na ziweze kufanya biashara ya mwani.

Habari Kubwa