Wakulima pareto waonywa mawakala vishoka

29Jul 2021
Grace Mwakalinga
Mbeya
Nipashe
Wakulima pareto waonywa mawakala vishoka

WAKULIMA wa zao la pareto katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya wametahadharishwa kujiepusha na mawakala feki ‘vishoka’ ambao wananunua zao hilo kwa wakulima kisha kuliuza bila kujali ubora hivyo kusababisha kushuka thamani kiwandani.

Tahadhari hiyo ilitolewa jana na mratibu wa huduma za ugani kutoka Kampuni ya Pareto nchini (PCT), Michael Bishubo, wakati kampuni hiyo ilipotembelea baadhi ya miradi ya ujenzi wa shule, zahanati na daraja na kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Bishubo alisema wapo baadhi ya watu ‘vishoka’ ambao wanawafuata wakulima shambani kisha kununua zao la pareto kwa Sh. 2,700 kwa kilo na kisha wao kwenda kuiuza kwa wakala bei hiyo hiyo.

“Vishoka wananunua bei hiyo hiyo na wao wanaenda kwa mawakala wetu kuuza bei hiyo kwa kilo sasa unajiuliza kuwa wanapata faida gani, lakini ukiangalia wanauza pareto ambayo haina ubora, ina mawe na takataka nyingine ambazo zinaongeza uzito kwenye mizani.’’

“Lakini kwa kuwa mawakala wetu wanalipwa kwa kamisheni wakishapekelewa kwenye vituo vyao wanachukua mzigo kama ulivyo bila kujua kuwa umechakachuliwa hali ambayo inaleta usumbufu kiwandani,’’ alisema.

Akizungumzia msaada, alisema kampuni ya PCT ni sehemu ya jamii kwa kuwa inafanya kazi na watu, hivyo imeamua kushirikiana na wanakijiji katika ujenzi wa vyoo vya Shule ya Msingi Itaga, Zahati ya Pashungu na ujenzi wa daraja la Izumbwe Two kwa kutoa mifuko ya saruji, mabati na fedha tasilimu.

Mkurugenzi wa PCT, John Power, alisema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani katika maeneo zinakofanyika shughuli za kilimo cha pareto.

Power alisema kampuni yake iko tayari kuongeza bei ya pareto kutoka Sh. 2,700 hadi kufikia Sh. 3,000 ikiwa wakulima wataongeza thamani ya zao hilo kuzalisha lenye ubora na linalofuata hatua muhimu za kilimo hicho.

Diwani wa Itawa, Elia Mwampamba, alisema PCT imekuwa ikishirikiana na jamii katika maeneo yote wanayozalisha zao la pareto na kwamba wataendelea kushirikiana nao katika masuala mbalimbali.

Msaada huo utasaidia kukamilisha ujenzi wa vyoo vya shule ya msingi Itaga, Zahanati ya Pashungu na ujenzi wa daraja la Mzumbwe Two lililobomoka kutokana na mvua za msimu uliopita.