Wakulima wa maharage wapewa mbinu za kisasa

29Jun 2017
Na Mwandishi Wetu
KARAGWE
Nipashe
Wakulima wa maharage wapewa mbinu za kisasa

WAKULIMA wa maharage katika Wilaya za Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera, wameshauriwa  kuacha kilimo cha mazoea badala yake walime kisasa ili kuongeza thamani ya zao  hilo na kuzalisha mazao mengine.

Wakulima hao ambao ni wanachama wa Shirika la Kaderes linalojishughulisha na kununua mazao kama kahawa na maharage kwa wakulima wilaya hizo walipewa ushauri huo juzi wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya kuanzishwa kwa shirika hilo.

Ushauri huo ulitolewa na mtafiti wa kilimo kutoka kituo cha utafiti  wa mazao Maruku, Manispaa ya Bukoba, Magdalena Wiliam, na kusema  kinachoshusha thamani ya mazao kwa wakulima  ni kulima kwa mazoea na kuchanganya mbegu zaidi ya moja.

Wiliam alisema wilaya hizo mbili za mkoa huu ndizo zinazozalisha maharage kwa wingi nchini huku Tanzania ikiwa nchi ya tano Afrika kwa uzalishaji wa zao hilo.

 Alisema kilimo cha tija kinawezesha kupata masoko ya nje na dani kwa kuuza kwa bei nzuri zao hilo na mbegu zake.

Festo Kagurusi, mkulima wa kilimo ambacho hakitumii madawa ya viwandani katika Kijiji cha Kikukuru wilayani Kyerwa, alisema mkulima inampasa kujikita katika kilimo hai kwani ndicho kitampatia  uhakika wa kupata vyakula bora ambavyo havina kemikali.

”Tangu mwaka 2010 nilianza kunufaika na kilimo hai ambapo nimekuwa nikilima ekari moja na nusu na kupata magunia  kuanzia 3-9 na kilo moja ya maharage ya aina ya mbegu  ni shilingi 4,000,” alisema Kagurusi.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Kaderes, Leonardi Kachebonaho,  kwa miaka mitano ijayo shirika limepanga kumpatia uwezo kija mwenye kutambua umuhimu wa kilimo kwa kuweka mashamba darasa ambayo atakwenda na kujifunza zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa ambaye alikuwa mgeni rasmi, Shaaban Lissu, alisema ili wakulima wapate mafanikio, waache kilimo cha holela na wakurugenzi wahakikishe kila kata ina mtaalamu wa kilimo na wawafuatilie  na kuhakikisha wanafanya kazi.

Habari Kubwa