Wakulima wa tangawizi Same wataka tume kuchunguza mitambo

27Jun 2016
Godfrey Mushi
Same
Nipashe
Wakulima wa tangawizi Same wataka tume kuchunguza mitambo

BAADHI ya wajumbe wa Bodi ya Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Tangawizi, Mamba-Myamba wilayani Same.

Wamemtaka Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk. Charles Tizeba, kuunda timu ya watalaam itakayochunguza kiini cha mitambo ya kiwanda cha kusindika zao hilo kushindwa kufanya kazi, licha ya kupewa taarifa zinazoacha maswali mengi.

Wanaushirika hao, walieleza kutoridhishwa kwao na majibu yaliyotolewa na waziri huyo mwishoni mwa wiki, wakati akijibu swali la Mbunge wa Same Mashariki, Nanghenjwa Kaboyoka, aliyehoji tatizo la wananchi wa jimbo hilo kukosa soko la uhakika kutokana na zao hilo kutoongezewa thamani.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Yonazi Yohana, alisema taarifa zinazotolewa kwa viongozi wa kitaifa zinaacha maswali kwa kuwa mpaka sasa mtambo wa kukaushia tangawizi ambao una matatizo makubwa ya kiufundi haujaondolewa kiwandani, huku mitambo mingine mitatu ukiwamo ule wa kukata vipande vya tangawizi, ikiwa imefanyiwa matengenezo, lakini haijajaribiwa.

“Tangu nilipoitwa na kuambiwa nimechaguliwa kuwa mwenyekiti wa bodi mwaka 2015 hadi leo, mitambo hii inasumbua na ni kama inasababisha hasara kwa wakulima kwa sababu wanauza tangawizi kwa bei ya hasara. Mimi nataka itumwe timu ya watalaam wafanye utafiti ni kwa nini mitambo haifanyi kazi,” alisema Yonazi.

Kwa upande wake, mjumbe wa bodi hiyo, Rashid Mwanyika, aliliambia Nipashe jana kuwa taarifa za kukamilika kwa mitambo hiyo na kwamba kinachosubiriwa sasa ni makabadhiano, zina walakini, kwa kuwa wao kama wajumbe wa bodi, hawana taarifa ya kukamilika kwake, zaidi ya kuiona baadhi yake ikiwa kiwandani.

“Kwanza tangu kizinduliwe hatujawahi kuzalisha tani 100. Ubovu wa mitambo hiyo umechochea kushuka kwa uzalishaji wa tangawizi kiwandani kutoka tani tisa, hadi kufikia tani 1.2 kwa siku. Na baadhi ya mitambo inatumia mafuta machafu ya vilainishi (used oil) kwa ajili ya kujiendesha,” alisema.

Katika majibu yake, waziri huyo alisema taarifa alizozipata kutoka mkoani Kilimanjaro zinaeleza kuwa mitambo ya kiwanda hicho iliyokuwa ikifanyiwa matengenezo imekamilika, na kinachosubiriwa sasa ni makabidhiano.

Hata hivyo, wakati serikali ikidai mitambo hiyo imekamilika na inasubiri makabidhiano, wakulima wa tangawizi bado wanaendelea kusotea madai yao ya zaidi ya Sh. milioni 200.

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa