Wakulima wa viungo wazidi kung’ara EU

11Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Wakulima wa viungo wazidi kung’ara EU

​​​​​​​BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) Tanzania, Manfredo Fanti, ameeleza kuridhishwa na utekelezaji wa mradi wa viungo visiwani Zanzibar na kwamba unaweza kuwa mkakati wa kuondoa umaskini.

Aidha, Fanti alisema ana matumaini makubwa kuwa mradi wa kilimo cha mboga, matunda na viungo utapunguza na hata kuondoa umaskini kwa wakulima wengi.

Aliyasema hayo wakati wa ziara maalumu ya kutembelea baadhi ya mashamba ya wakulima katika shehia ya Kizimbani na Biguni kisiwani Unguja.

 

Alisema kilimo hicho ni miongoni mwa sekta muhimu ambayo ikitumiwa vyema itabadilisha maisha ya wakulima na kuzalisha kwa wingi, mazao yenye ubora na kupata soko la uhakika.

 

Aliwataka wakulima hao wasikate tamaa na waendelee kutumia fursa zinazopatikana kupitia mradi wa viungo na kwamba

ushiriki mkubwa na utayari wa kujifunza waliouonyesha wakulima wengi unatia moyo.

Alisema anaamini kwamba elimu waliyopata wataitumia vyema kuendeleza kilimo chao kwa manufaa ya jamii, na taifa kwa ujumla.

Aidha, aliwataka wanufaika wa mradi kuitumia fursa hiyo kama sehemu muhimu ya kujifunza na kuongeza uelewa kupitia aina mbalimbali mpya za kilimo ambazo hazikuwa zikitumiwa awali.

 

Baadhi ya wanufaika wa mradu huo Haji Abdallah Abeid, mkulima wa vanila, alisema elimu aliyoipata kupitia mradi wa viungo imemwezesha kuimarisha kilimo chake na ameanza kuona mabadiliko makubwa ya jinsi ya ulimaji wake kuanzia utayarishaji shamba, kupanda na anaamini atavuna mazao mengi na bora.

 

“Nimefanya shughuli za kilimo hiki kwa miaka mingi lakini kwa njia za kienyeji ambazo hazikuniwezesha kupata mafanikio ninayoyatarajia, lakini sasa kupitia elimu hii na utaalamu tunaoupata kutoka mradi wa viungo ninaamini ndoto yangu itatimia,’’ alisema Haji.

 

Alieleza kuwa kupitia mradi huo wa viungo amejifunza njia mpya za kilimo hicho cha vanila na tayari ameanza kuzifanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuanzisha shamba jipya ambalo tayari ameshaotesha miche zaidi ya 200.

 

Alisema kupitia mashamba darasa yanayoanzishwa kila shehia na mradi wa viungo yatawawezesha kwa kiasi kikubwa kuendelea kujifunza mbinu mbalimbali ambazo zitaleta mafanikio makubwa kwa wakulima wa mboga, matunda na viungo ambao ndiyo wanufaika wa mradi huo.

 

Akizungumzia kuhusu hali ya soko la vanila alisema kwa sasa kilo moja ya vanila wanauza kwa Sh. milioni 1.6 hivyo kupitia mradi huo ana imani soko la bidhaa hiyo litakuwa zaidi na wataongeza uzalishaji na ubora wake.

 

Kwa upande wake mkulima wa matunda wa shehia ya Binguni Namri Najim, alisema mfumo mpya wa kilimo unaozingatia elimu utaleta tija kwao na kuzalisha bidhaa nyingi zaidi.

 

Mkulima huyo ambaye anayejihusisha na kilimo cha mapesheni na mapapai anasema pia kupitia mfumo huo watakuwa na uhakika wa masoko kutokana na kuzalisha bidhaa bora zenye kiwango zinazohitajika ndani na nje ya Zanzibar.

 

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa Utekelezaji Mradi, Amina Ussi Khamis, alisema ujio wa Balozi Fanti kutembelea mradi huo una manufaa makubwa kufuatilia kile ambacho wamewekeza kwa nia ya kuwasaidia wananchi wa Zanzibar.

 

Alisema anaamini wakulima wataitumia fursa hiyo na kuwataka waongeze kasi ya kujifunza zaidi kupitia mashamba darasa yaliopo katika shehia zao kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa bidhaa bora.

 

Mradi huo unaofadhaliliwa EU, unatekelezwa kwa miaka minne visiwani Zanzibar katika shehia 60 za Unguja na Pemba ambao umelenga kuwafikia wanufaika 57,974.

Habari Kubwa