Wakulima walia bidhaa kukosa soko

25Mar 2020
Godfrey Mushi
Moshi
Nipashe
Wakulima walia bidhaa kukosa soko

WAKULIMA wa vijiji vya pembezoni vinavyopakana kati ya Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro na Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, wameiomba serikali kutatua tatizo la muda mrefu la ukosefu wa soko la uhakika la mazao ya mboga na nafaka.

Kukosekana kwa soko hilo, kunadaiwa kusababisha hasara kubwa kwa wazalishaji ambao hutumia gharama kubwa kuzalisha na kushindwa kuuza.

Ombi hilo lilitolewa jana kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Msitu wa Tembo na Londoto vilivyoko wilayani Simanjiro, na Langasani, Mikocheni na Arusha Chini vilivyoko wilayani Moshi.

Mmoja wa wakulima hao, Beda Msumba, mkazi wa Msitu wa Tembo, alisema tatizo la upatikanaji wa masoko ya uhakika wa mazao wanayolima, limekatisha wengi ndoto zao kutokana na hasara wanayoipata.

“Kutokana na hiyo hasara, wengi wetu tunashindwa kumudu gharama za kilimo na kulazimika kulima kilimo cha mazoea kisichokuwa na tija, badala ya kuendelea na kilimo cha kisasa.

“Tatizo la msingi kwetu linaanzia hapo ambapo tunashindwa kupata masoko ya uhakika na kusababisha kushindwa kuendelea kulima misimu inayofuata. Wakati mwingine tunalazimika kutumia mbegu ambazo tayari zilikuwa zimepandwa kama mazao ya kuuza na kuvuna mavuno kidogo," alilalamika.

Francis Mfuru, mkazi wa Londoto, alisema kwa muda mrefu tatizo la upatikanaji wa pembejeo bora na masoko, limekuwa ni kikwazo kikubwa cha wakulima kupiga hatua za maendeleo, hivyo wakaiomba serikali na wadau wa maendeleo kuwatafutia masoko ya uhakika na pembejeo bora.

Saida Ramadhan, mkazi wa Langasani, alisema: “Kwa sasa tunaiomba serikali kuangalia uwezekano wa kutoa vibali vya kusafirisha mazao nje ya nchi ili wakulima wanufaike na kurejesha mikopo katika taasisi za kifedha kama ombi hili litachelewa kutekelezwa.”

Akiwajibu wananchi hao, Ofisa Masoko wa Shirika Lisilo la Kiserikali la Rikolto, linalotoa elimu ya kilimo na mnyororo wa thamani, Eliud Ng’umbi, alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, taasisi hiyo imeanza kutoa mafunzo kwa wataalamu pamoja na wakulima wa maeneo hayo.

“Pamoja na kuwaunganisha na taasisi za fedha kupata mikopo ya kilimo, lakini tunawaunganisha na masoko kwa kuingia mikataba ya wakulima na wanunuzi kununua mazao yao," alisema.

Habari Kubwa