Wakulima walia na wafugaji kushambulia mashamba yao

08Nov 2016
Ashton Balaigwa
KILOSA
Nipashe
Wakulima walia na wafugaji kushambulia mashamba yao

WAKULIMA wa Kata ya Ludewa na Peapea wilayani Kilosa, wapo hatari kukumbwa na njaa baada ya mashamba yao kuharibiwa na mifugo.

Wakulima hao walitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Kijiji cha Ludewa, mbele ya Mbunge wa Jimbo la Kilosa, Mohamed Bawazir na viongozi wa CCM, wilayani humo.

Akiongea katika mkutano huo, mmoja wa wakulima hao kutoka Kijiji cha Ludewa, Said Mdomowazi, alisema hali imekuwa mbaya kwa kuwa wanaishi kwa kula mlo mmoja kutokana na mazao yao kulishwa mifugo inayoingizwa na wafugaji kwa makusudi.
 
Alisema licha ya kufanya jitihada ya kuifukuza mifugo hiyo inapoingia katika mashamba hayo, wamekuwa wakiambulia kupigwa na wafugaji hao na kutishiwa sime.

John Songa, mkulima kutoka kata hiyo, alimuomba mbunge huyo kufikisha malalamiko yao kwa Rais Dk. John Magufuli, kwa kuwa uongozi wa wilaya na mkoa, umeshindwa kutatua tatizo hilo la wafugaji kulishia mashamba ya wakulima.

Eliza Zamayoni, alisema mifugo hiyo imekuwa kero na kikwazo cha maendeleo kwa wakulima huku wanapojaribu kuiondoa, wakitishiwa kufanyiwa vitendo vya kinyama ikiwamo kubakwa.

Mbunge Bawazir, alisema anakusudia kuambatana na baadhi ya wananchi kwenda kumuona Rais kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, alisema ameshawachukulia hatua ikiwamo kuwafikisha katika vyombo vya usalama, wafugaji wote wanaoingiza mifugo katika mashamba ya wakulima.

Alisema kesi za wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima zimeanza kuhukumiwa katika mahakama ya wilaya hiyo.

Habari Kubwa