Wakulima wanufaika mkopo wa pembejeo

11Feb 2019
Allan lsack
Arumeru
Nipashe
Wakulima wanufaika mkopo wa pembejeo

WAKULIMA kutoka vijiji 21 vya Halmashauri ya Meru, wamenufaika na mkopo nafuu wa pembejeo za kilimo kutoka shirika la kimataifa la One Acre Fund.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa zoezi la ugawaji wa pembejeo kwa wakulima, wilayani humo, uliofanyika katika Kata ya Kikatiti mwishoni mwa wiki, msemaji wa shirika hilo, Maico Machela, alisema wameshatoa mkopo wa pembejeo za thamani ya Sh. milioni 580.9 na kuwanufaisha wakulima zaidi ya 2,000.

Aliongeza tangu kuanzishwa shirika hilo, mwaka 2013, limewafikia wakulima wapatao 52,000 na lengo ni kuwafikia wakulima 100,000 ifikapo mwakani.

"Katika wilayani ya Arumeru tunahudumia halmashauri mbili, Meru na Arusha Vijijini, ambapo Halmashauri ya Meru tumetoa tani 320 za mbolea, mbegu za mahindi tani 18, taa za umeme wa nguvu ya jua 716, mifuko ya kuhifadhia nafaka 5,478, mbegu za miti 3,355 na chokaa vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 580.9," alisema.

Aidha, alisema shirika hilo, lilianzia mkoani Iringa na baadaye mikoa ya Njombe, Songwe, Mbeya na mwaka huu limeingia mkoani Arusha katika Wilaya ya Arumeru.

Alisema wakulima wamekuwa wakikopeshwa pembejeo za mbegu za mahindi, mbolea za kupandia na kukuzia mazao, taa za umeme wa nguvu ya jua, mifuko ya kuhifadhia mazao na baadaye hurejesha mkopo kidogo kidogo wakati wa kuuza mazao yao.

Alisema shirika hilo linafanya kazi katika nchi za Afrika Mashariki na linahudumia wakulima katika nchi za Rwanda, Burundi, Zambia, Malawi na mwaka 2012 liliingia nchini Tanzania.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro, alilipongeza shirika hilo, kwa hatua yake ya kuwapatia mikopo wa pembejeo wakulima waliopo katika wilaya yake jambo litakalo wanufaisha kufikia kilimo chenye tija kwa wananchi wake.

Aliwataka maofisa ugani wilayani humo, kuhakikisha wanasimamia mradi wa shirika hilo, kwa kuwatembelea wakulima na kuwapatia elimu juu ya matumizi sahihi ya pembejeo walizopewa.

Diwani wa Kikatiti, Elisa Mungure, alisema katika kata yake wakulima wamenufaika na pembejeo zenye thamani ya Sh. milioni 51, zilizotolewa na shirika hilo, pamoja na taasisi nyingine zilizowekeza kwenye kata hiyo, kwa ajili ya kuwanufaisha wakulima kulima kilimo cha kisasa na chenye tija.

Habari Kubwa