Wakulima wapewa ushauri wa bure

09Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Wakulima wapewa ushauri wa bure

WAKULIMA nchini wameshauriwa kufuata taratibu kutoka kwa wataalamu wa zana za kilimo hususani wanapotaka kununua zana za kilimo ili kuepukana na hasara za kununua zana feki au zisizostahili kwa kilimo husika.

Ushauri huo ulitolewa mjini hapa mwishoni mwa wiki na mkurugenzi ya kampuni inayotoa mikopo ya zana za kilimo yakiwamo matreka na mashine za kuvuta maji ya Kabugamo, Ndallo Kabuche, wakati akizungumza na Nipashe kuhusiana na malalamiko ya wakulima kuuziwa zana zilizo chini ya kiwango.

Alisema baadhi ya wakulima wanapotaka kununua zana za kilimo kama materekta au mashine hushindwa kumueleza muuzaji wa zana hizo kulingana na hali halisi ya mahitaji yake, hivyo hununua zana kwa bei ndogo wakati uzalishaji anaotaka kuufanya ni mkubwa.

Alisema baadhi ya wakulima wanataka kupiga hatua na kuendelea na kilimo cha kisasa lakini hawafuati maelekezo ya zana husika kulingana na mazingira ya kilimo chake hali inayoathiri uzalishaji wa mazao yake.

“Unapotaka kununua treka lazima utoe maelezo ya ukubwa wa sehemu ya shamba lako na aina ya udongo, kwa wasindikaji wanatakiwa kueleza ukubwa wa bidhaa wanazotaka kuzalisha ili wapate mashine inayostahili kuzalisha bidhaa husika,” alisema.

Kabushe alisema katika kuboresha kilimo nchini hasa kwa wakulima wadogo na kati, kampuni hiyo imekuwa ikitoa mikopo ya masharti nafuu, lakini urejeshaji wake umekuwa ukichukua muda mrefu.

Naye Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (Sido) mkoani Dodoma, Abel Mapunda, alizitaka kampuni za kukopesha zana za kilimo kutoa mafunzo kwa wakulima na kutembelea maeneo ya uzalishaji ili kutoa ushauri, badala ya kusubiri wateja kwenda kununua bidhaa.

Alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likidhibiti na kuangalia ubora wa zana za kilimo zinazoingia kutoka nje ili kuhakikisha zinakuwa bora na zina alama ya kitamataifa.

Habari Kubwa