Wakulima watakiwa kusoma alama za nyakati

15Mar 2017
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Wakulima watakiwa kusoma alama za nyakati

WAKULIMA wa viazi lishe wametakiwa kutunza mbegu na kusoma alama za nyakati, ili waweze kuendana na soko na kuimarisha afya zao.

Rai hiyo ilitolewa jana mjini hapa na wataalamu wa Shirika la Recoda, wakishirikiana na CIP, wakati wakitoa elimu kwa baadhi ya viongozi wa vikundi vya wakulima waliotoka katika wilaya mbalimbali za mikoa ya Kilimanjaro, Singida, Arusha na wenyeji Manyara.

“Ni vizuri watu wakawa na mkakati wa kutunza mbegu, ili kuepuka kukosa mbegu wakati wa kupanda na ni vizuri kusoma alama za nyakati, ili baadaye msianze kulalamikia soko,” alisema Meneja mradi viazi lishe Recoda, Bryson Sabuni.

Alisema wakulima wengi wanazalisha viazi lishe kipindi cha mvua nyingi, hivyo kukosa wateja na kuwashauri kuzalisha pia wakati wa kiangazi ili kupata soko zuri.

Aidha, alisema wakifanya hivyo watasaidia kupishana kwa misimu ili kuwa na uhakika wa mbegu ambazo zitaendana na kaulimbiu ya shirika, “Mazao lishe huondoa udumavu na njaa iliyojificha”.

Mtaalamu wa kituo cha utafiti Kibaha, Mariam Kilima, aliwashauri wakulima wanaolima viazi hivyo kibiashara wasikate viazi vyao wakati wa kuvuna.

Kilima alisisitiza umakini katika kuvihifadhi mara baada ya wakulima kuvuna viazi hivyo ambavyo vitawaongezea kipato na kuwaletea maendeleo ya haraka ukilinganisha na wanaolima bila kufuata utaalamu.

“Baada ya kuvuna chimba shimo na uzungushie majani makavu pembeni ili visiharibike, unaweza kuvitunza kwa miezi
hadi mitano na kufanya hivyo ni kuvirefushia maisha kusubiri bei,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Recoda, Dominick Ringo, alisema, mpango huo ulianza rasmi mwaka 2013 kwa ajili ya
kutoa teknolojia kwa wakulima wadogo waliyowapa wakulima, nao wataenda kuwafundisha wengine.

Habari Kubwa