Wakulima wawatuhumu viongozi kuuza ardhi

27Feb 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Wakulima wawatuhumu viongozi kuuza ardhi

WAKULIMA wa vijiji 11 vya tarafa ya Duthumi wilayani Morogoro, mkoani hapa, wamelalamikia viongozi wa Jumuiya ya Wanyamapori kwa madai ya kuuza eneo lililotengwa katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa vijiji hivyo, kwa wafugaji.

Waziri wa Kilimo Mwigulu Nchemba.

Wakulima hao wameeleza kuwa tayari wafugaji hao wameshafanya makazi ya kudumu na hivyo eneo hilo kushindwa kupangiwa matumizi bora ya ardhi.

Akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya wenzake, mkazi wa kijiji cha Duthumi, Lidya Mwambasa, wamemtuhumu mwenyekiti wa jumuiya hiyo kwa kuhusika katika kushiriki uuzwaji wa eneo hilo.

Alisema wamekuwa wakifuatilia mara kwa mara kuhuau eneo hilo, lakini wameishia kufukuzwa na mwenyekiti huyo kwa kutumia askari wanyamapori.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Bonye Yahaya Kidoto na Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho,walithibitisha kuwapo kwa mgogoro huo na kudai mwenyekiti huyo amekuwa akitumia madaraka yake vibaya ikiwamo kuwanyanyasa wakulima.

Kidoto aliitaka serikali kuingilia kati suala hilo kuepusha mgogoro unaoweza kuibuka kati ya wakulima na wafugaji.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Shaban Kolahil, akijibu malalamiko hayo kwa njia ya simu alikanusha tuhuma hizo.
Alisema eneo hilo halijauzwa na kuliomba jeshi la polisi kuongeza nguvu ili kuwaondoa wafugaji waliovamia.

Habari Kubwa