Walalamika kuuziwa Vitambulisho vya Taifa 10,000/-

01May 2019
Jaliwason Jasson
MANYARA
Nipashe
Walalamika kuuziwa Vitambulisho vya Taifa 10,000/-

WANANCHI wa Mtaa wa Nyunguu katika Halmashauri ya Mji wa Babati, Mkoani Manyara, wamelalamikia uongozi wa mtaa huo, kuwalazimisha kulipia Sh.10,000 ili waweze kupatiwa Vitambulisho vya Taifa.

Malalamiko hayo waliyatoa jana mjini hapa, wakati wakizungumza na Nipashe kuhusu kadhia hiyo ambayo inaongozwa na ofisi ya mtaa kupitia kwa Ofisa Mtendaji na baadhi ya wajumbe wa serikali ya mtaa.

Mmoja wa wakazi hao, Mustafa Rwamcho, alisema alienda siku moja ofisi ya mtaa huo ili aweze kuchukua kitambulisho chake, lakini alinyimwa kwa madai kwamba anatakiwa achangie mchango wa Shule ya Sekondari Babati Day, Sh. 10,000.

“Mimi baada ya kunidai nitoe fedha niliamua kukiacha na mpaka sasa sijarudi tena na sijui itakuwaje, maana hiki kitambulisho kinahitajika, mfano ukienda nje ya nchi unaweza ukatakiwa uonyeshe kitambulisho hicho, ili kuthibitisha uraia wako,’’ alisema Rwamcho.

Aidha, alisema kwa kuwa hali yake kiuchumi haikuwa nzuri, alikiacha kitambulisho hicho huku akisema kuendelea kukikosa italeta madhara zaidi kwa kuwa mamlaka ya mawasiliano inawataka watumiaji wa simu kusajili laini za simu wawe na vitambulisho hivyo.

“Kwa kuwa rais Magufuli alishasema vitambulisho hivi ni bure,namuomba atusaidie kuwawajibisha viongozi wa namna hii, ambao wanatuuzia vitambulisho wakati vinatakiwa kutolewa bila malipo ya aina yeyote,’’ alifafanua. 

Mkazi mwingine, Leah Mapinda, alisema anashangaa ofisi ya mtaa, kuwatoza fedha hizo huku akidai mdogo wake alilipishwa fedha hiyo na kusisitiza kuwa endapo wataendelea kuwatoza wananchi ambao baadhi hawana uwezo hawatapata vitambulisho.

Mapinda alihoji waliopewa mwaka jana hawakutozwa Sh.10, 000, lakini mwaka huu viongozi wanaanza kuwatoza fedha hiyo, ilhali ni haki yao kupata Vitambulisho vya Taifa.Musa Rajab, aliiambia Nipashe kuwa viongozi kuwatoza fedha wananchi katika kuwapatia vitambulisho ni kukiuka maelekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani Nchi, Kangi Lugola na rais John Magufuli wanapokuwa kwenye ziara zao.Nipashe ilipoutafuta uongozi wa mtaa wa Nyunguu, iliwekewa masharti ya kuwa na kibali cha kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Babati ambacho ilipewa kwa maneno.

Hata hivyo, alifuatwa ofisini kwake Ofisa Mtendaji huyo, Nipashe iliambiwa kwa njia ya simu kuwa yupo mtaa jirani wa mji mpya, akiwa na wenzake wakikusanya michango.

Alipofuatwa katika mtaa huo, Ofisa Mtendaji husika, aliyeshirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bagara, alimtaka mwandishi aonyeshe kibali cha maandishi badala ya maneno.Naye mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Fortunatus Fwema, alipoongea na Nipashe ofisini kwake, alisema uongozi wa kata au mtaa watakuwa wamejiwekea utaratibu huo na kama kuna wananchi wana malalamiko ya kutozwa fedha, wafikishe taarifa ofisini kwake au kwa mkuu wa wilaya. 

Nipashe ilifika ofisi ya Nida ili kujua kama wanafahamu jambo hilo, Ofisa Msimamizi wa zoezi hilo mkoani hapa, ambaye hakuwa tayari kuzungumza wala kutaja majina yake alidai mpaka apewe ruhusa na Mkurugenzi wa Nida. Alisema uongozi wa mtaa huo kuwalipisha fedha siyo sahihi, maana Vitambulisho vya Taifa vinatolewa bure.

Alisema serikali imekwisha gharamia hivyo watu wote wanatakiwa kupewa bure vitambulisho pasipo vikwazo vyovyote na haitakiwi kuchangisha michango, kwa kutumia kigezo cha kuwanyima wananchi vitambulisho vyao.

Aliongeza kuwa lengo la kuwapatia watendaji vitambulisho hivyo, ili wavigawe kwa wananchi ni kuwasaidia kuwasogezea huduma karibu, lakini kama imekuwa kinyume chake alisema ataongea na Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ndiye muajiri wa maofisa watendaji, kuona jinsi ya kuwazuia, ili wasiendelee kuwauzia vitambulisho hivyo kwa kisingizio cha michango. 

Habari Kubwa