Walia kodi dagaa kupanda

26Mar 2020
Anthony Gervas
Mwanza
Nipashe
Walia kodi dagaa kupanda

USHIRIKA wa wauza samaki katika soko la kimataifa mwaloni jijini Mwanza (Uwasa), umeiomba serikali kupunguza kodi ya dagaa, baada ya wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kushindwa kumudu na kuacha kwenda kununua dagaa katika soko hilo.

Mwenyekiti wa Soko hilo, Fikri Magafu, alisema jana kuwa tangu Julai mwaka jana, serikali ilipandisha kodi ya samaki hao wadogo kutoka Dola 0.16 (Sh. 368) hadi Dola 0.2 (Sh. 460) kwa kilo.

“Serikali ilipandisha kodi ya dagaa tangu mwaka jana na kusababisha wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kushindwa kumudu na kuacha kuja kununua tena dagaa, hivyo tunaiomba ishushe kodi hiyo ili wafanyabiashara hao warudi kununua," alisema.

Magafu alisema wafanyabiashara hao kutoka nchi za Burundi, Uganda, Rwanda, Malawi, Zambia na DRC, wamelazimika kuacha kwenda kununua dagaa kwenye soko hilo na kuelekeza mitaji yao kwenye masoko ya nchi za Ethiopia, Msumbiji, Kenya na Zanzibar.

Alisema pamoja na serikali kuahidi kwa muda mrefu kushusha kodi hiyo, bado haijafanya hivyo na kwamba hivi sasa dagaa wameshuka soko lake, gunia likiuzwa kuanzia Sh. 90,000 hadi 110,000, wakati awali liliuzwa kuanzia Sh. 160,000 hadi 180,000.

"Biashara ya dagaa haina bei elekezi bali ni soko huria, kuna wakati inapanda kutokana na kuadimika lakini wakati mwingine inashuka kutegemea na nyakati hizo kuwa nyingi zaidi na kukosa wateja," alifafanua.

Alisema kwa hivi sasa, dagaa wanasafirishwa kwenda kuliwa ndani ya nchi katika mikoa ya Arusha, Mbeya na Dar es Salaaam kutokana na wanunuzi wa nje kuacha kwenda Mwanza kuwanunua.

Habari Kubwa