Walia ushuru mkubwa samaki

14Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Buchosa
Nipashe
Walia ushuru mkubwa samaki

WANUNUZI wa sangara katika Halmashauri ya Buchosa, Sengerema mkoani Mwanza, wameilalamikia halmashauri hiyo kuwatoza ushuru wa Sh. 200 kwa kila kilo moja.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanunuzi wa Samaki hao, Gregory Kazimbo, alisema juzi kuwa ushuru huo ni mkubwa kwa sababu kwenye mialo wanalazimika kununua kwa Sh. 3,500 kwa kilo na kuuza viwandani kwa Sh. 4,000.

"Tumepeleka maombi yetu katika halmashauri hiyo ili Baraza la Madiwani litusaidie kubadilisha ushuru huo mkubwa kwa kila kilo ya samaki Sh. 200. Tunaomba iwe angalau Sh. 30,” alisema Kazimbo.

Kazimbo alisema umoja huo ulianzishwa kutoka katika mialo ya Mkoamani, Nyakaliro, Nyarusenyi, Ntama, Mchangani, Mbugani, Kanyara, Chembaya, Kabiga na Kahunda.

Alisema awali walikuwa wakilipa ushuru wa jumla kwa kila tripu moja ambayo ilikuwa Sh. 100,000 lakini sasa umebadilika jambo ambalo linawaumiza katika biashara hiyo na kuwakosesha faida.

Hata hivyo, alisema wanaiomba halmashauri kuendelea kuwatoza ushuru wa jumla wa Sh. 150,000 badala ya sasa ambao unawaumiza.

Alisema umoja huo hauridhiki kutozwa ushuru huo kutokana na changamoto nyingi zinazowakabili ikiwamo michango ya kijamii, kulipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA0, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), ushuru wa viwandani na leseni za ukusanyaji samaki na usafirishaji.

Aidha, Kazimbo alisema bado ziko gharama nyingi zinawakabili katika jamii ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa ujenzi wa shule, zahanati, mialo, usafi wa mazingira, ulinzi wa mialo, kulipa vibarua, mafuta na vifaa vya kuendeshea vyombo hivyo, matengenezo na usafirishaji.

Habari Kubwa