Walima tumbaku waipa serikali kazi ya ziada

02Dec 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Walima tumbaku waipa serikali kazi ya ziada

SERIKALI imelazimika kufanya kazi ya ziada ya kutafuta soko la tumbaku baada ya  wakulima wa zao hilo nchini kuzalisha kilo 69,757,425 katika msimu uliopita, hivyo kuwa zaidi ya  lengo la uzalishaji kwa mujibu wa mikataba ambao ilikuwa kilo 57,305,127.

wakulima wa tumbaku wakizihifadhi kwenye ghala.

Kutokana na hatua hiyo, serikali imepata kazi ya ziada kuhakikisha inawasaidia wakulima hao kupata soko la kilo 12,452,298 zilizozalishwa nje ya mikataba.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, alipozungumza na waandishi wa habari.

Alisema tumbaku iliyonunuliwa mpaka mwisho wa msimu huo wa mwaka 2018/2019 ndani ya mikataba ni kilo 60,691,972.21 zenye thamani ya dola za Kimarekani 92,927,331.79 sawa na asilimia 105.9 ya lengo.

“Jitihada za Wizara ya Kilimo kushirikiana na Bodi ya Tumbaku zilifanikiwa kushawishi kampuni ya Alliance One na Premium Active kununua tumbaku kilo 6,305,000, kuongeza kilo toka 4,200,000 hadi 7,400,000, mpaka sasa, ununuzi wa tumbaku hiyo iliyozidi malengo ya uzalishaji umefikia kilo 8,107,221 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 6,330,174,” alisema.

Alisema tumbaku iliyobaki kwa wakulima bila mnunuzi ni kilo 3,345,077 katika mkoa wa Tabora na kiasi kidogo Ushetu Shinyanga, ununuzi umekamilika kwa 100% mkoa wa Mbeya, Songwe, Kigoma,Singida, Iringa, Ruvuma na Katavi,” alisema.

Waziri alibainisha kuwa wizara yake imeendelea  kuhakikisha tumbaku hiyo inanunuliwa yote toka kwa wakulima, mnamo Novemba 11, 2019 Kampuni mbili ambazo ni Copper Leaf Company na Tombwe Processing toka nchi ya Zambia, zimekbali kununua tumbaku iliyobaki kwa wakulima na tayari wamewasili nchini na wameanza kusaini mikataba kupitia vyama vya msingi vya ushirika.

“Kwa hatua hiyo tatizo la uwepo wa tumbaku iliyozalishwa nje ya mkataba msimu huu kwa wakulima wa tumbaku litakuwa limekwisha kabisa. Wananchi waendelea kulima mashamba kwa msimu unaokuja,” alisema.

Katika msimu wa kilimo 2019/2020 ambao masoko yake yataanza mwezi Mei 2020, kampuni za ununuzi zilizopo nchini ambazo ni Alliance One Tanzania, Premium Active Tanzania na Japan Tobacco International zimetoa mikataba ya kilo 42,225,985.

“Tayari wakulima wapatao 33,000 wameomba kusajiliwa na Bodi ya Tumbaku kutokana na uzalishaji huo, uzalishaji huo ni mdogo na hivyo unaacha wakulima takribani 16,000 bila kulima tumbaku msimu huu,” alisema.

Alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo wizara kupitia Bodi ya Tumbaku ilianzisha jitihada za kutafuta masoko mengine ili kuziba pengo la kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco – TLTC ambayo haijatoa makisio ya uzalishaji msimu huu.

Alisema kampuni nne mpya tayari zimeonesha nia ya kununua tumbaku ya Tanzania msimu ujao. Kampuni hizo ni Magefa Growers Ltd itanunua kilo 5,500,000 Transafricque kupitia kampuni ya kizawa ya Grand Tobacco Growers Co. Ltd imeomba kununua kilo 9,000,000, Petrobena itanunua kilo 300,000 na Pachtec  Ltd imeomba kununua kilo 500,000.

Habari Kubwa