Walimu wanolewa kuongeza kiwango

28May 2019
Godfrey Mushi
SIHA
Nipashe
Walimu wanolewa kuongeza kiwango

CHUO Kikuu Kishiriki cha Katoliki Mwenge (Mwecau), kwa ushirikiano na Halmashauri ya Wilaya ya Siha kimeanza kuwanoa bongo, walimu 60 wa shule za sekondari za wilaya hiyo ambao watatumika kama injini ya kubadili taswira ya ufaulu katika mitihani ya kitaifa.

Katika kuhakikisha kiwango cha elimu kinapanda, serikali na wadau wa elimu wamekuwa wakiendesha mafunzo mbalimbali ili kuondoa tatizo linalosababisha kiwango cha elimu kushuka.

Ofisa Habari wa chuo hicho, Athanas Sing'ambi, aliieleza Nipashe jana kuwa walimu hao wanapatiwa mafunzo ya mbinu bora za ufundishaji shuleni.

"Nia yetu ni kuwawezesha walimu kuwa na uwezo mkubwa wa ufundishaji ili kuongeza uelewa kwa wanafunzi, dhana ni kwamba bila kuwanoa walimu katika baadhi ya masomo yanayoonekana kutofanywa vyema na wanafunzi inaweza kuwa ngumu kufikia malengo yanayotarajiwa," alisema.

"Gari linapotembea umbali mrefu kuna vitu vinalegea na kuchoka, hivyo huhitaji matengenezo au marekebisho ili liendelee na safari vizuri zaidi.

Kuna umuhimu kwa walimu kupatiwa mafunzo kazini ili awe na kasi ya ufundishaji na matokeo ya anachofundisha kiwe na tija," aliongeza.

Kwa nini kuna umuhimu wa walimu kunolewa, Sing'ambi ameeleza zaidi kuwa walimu wanahitaji mafunzo ya mara kwa mara kutokana na jinsi ulimwengu unavyobadilika. Kwa mfano, wanasayansi wametupa taarifa kwamba sayari ya Pluto haina sifa ya kuwa sayari, kwa sababu haina magimba yanayoizunguka, vile vile sayari nyingine imegunduliwa.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalifunguliwa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Valerian Juwal.

Mafunzo yanafanyika katika Shule ya Sekondari Magnificant yakishirikisha walimu 60 wa Shule za Sekondari za Siha.

Habari Kubwa