Waliokuwa wafanyakazi wa TTPL walilia mafao yao PPF

08Nov 2016
Ashton Balaigwa
MOROGORO
Nipashe
Waliokuwa wafanyakazi wa TTPL walilia mafao yao PPF

WALIOKUWA wafanyakazi wa msimu wa Kampuni ya kuchakata tumbaku (TTPL), Mkoa wa Morogoro, wameangua kilio wakiwa na baadhi ya watoto wao wakati walipoweka kambi ya muda katika Ofisi ya Mfuko wa Pensheni (PPF) Kanda ya Mashariki, kushinikiza kulipwa mafao yao.

Wafanyakazi hao wanaokadiriwa kuwa zaidi ya 1,000 waliweka kambi katika ofisi za PPF, kuanzia saa 1.00 asubuhi kabla ya ofisi hizo kufunguliwa kushinikiza kulipwa mafao hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari, katika ofisi hizo kwa niaba ya wenzake, mmoja wa viongozi wa wafanyakazi hao, Matabi Julius, alisema imewalazimu kufanya hivyo kutokana na PPF kushindwa kuwalipa mafao yao baada ya kumaliza msimu na kiwanda hicho.

Alisema kuwa Mfuko huo, ulifika katika kiwanda hicho mwezi Juni, mwaka huu na kuzungumza na wafanyakazi hao kuwa watakapomaliza msimu wao wa kazi katika kiwanda hicho, watalipwa fedha zao, lakini wanashangazwa kutolipwa hadi sasa. 

“Hawa viongozi wa PPF kabla ya kuanza msimu pamoja na mifuko mingine, walikuja kutoa elimu na ilikuwa mwezi Juni nakumbuka na kuahidi kulipa makato yetu, mara baada ya msimu kuisha na tumemaliza juzi Oktoba 31, lakini kila tukija kuulizia, hawatupi majibu yoyote na viongozi wanatukimbia, sasa tumeamua leo kukaa hapa hapa,” alisema.
 
Shida Kingali, aliyefika ofisi hizo akiwa na watoto wake, alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na mfuko huo kushindwa kutimiza ahadi zake za kuwapa mafao wakati walipokuja kuwaomba kujiunga.

Alisema wanashangazwa na PPF kushindwa kutimiza makubaliano hayo na kuwafanya kuendelea kuishi kwa shida wakati mifuko mingine imeshawalipa mafao yao wafanyakazi wengine wa msimu.

Nipashe, ilizuiliwa na kundi la wafanyakazi wa mfuko huo kuingia ofisini kupata ufafanuzi kwa madai kuwa meneja yupo nje ya ofisi na wenye mamlaka wa kuzungumzia suala hilo ni Makao Makuu ya PPF, jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa