Waliokwamisha maelfu ya leseni madini kuhamishwa

06Dec 2019
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Waliokwamisha maelfu ya leseni madini kuhamishwa

SERIKALI imemwagiza Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu Tume ya Madini, Gifti Kilimwomeshi, kuhakikisha watumishi watano wa Idara ya Leseni na Tehama makao makuu wanahamishiwa mkoani Tabora ndani ya siku tano kutokana na kufanya mgomo uliosababisha maombi ya leseni 3,410 kukwama.

Waziri wa Madini, Dotto Biteko, picha mtandao

Hayo yaliainishwa na Waziri wa Madini, Dotto Biteko, jijini hapa wakati akizungumza na waajiriwa wapya 116 wa tume hiyo ambao wameripoti na kupewa mafunzo kwa ajili ya kupangiwa vituo vya kazi .

Tukio hilo lililambatana na uzinduzi wa magari 10 yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya kazi mbalimbali.

Alisema, watumishi hao waliweka mgomo baridi na kusababisha mapato ya mwezi Oktoba na Novemba kushuka kutokana na mgomo huo uliosababisha leseni 3,410 kukwama huku wananchi wakibaki kulalamika.

Waziri alisema tume ilichukua watumishi wanne kutoka Tabora na kuwaleta jijini Dodoma kuja kufanya kazi wakati makao makuu kuna watumishi katika Idara hiyo ya leseni kisha wameweka mgomo baridi.

"Kwa serikali ya sasa hilo haliwezekani na halikubariki kila mmoja anapaswa kufanya kazi alipopangiwa," alisema Biteko.

"Wananchi wanalia kuna watu wanaweka mgomo baridi na kuacha kufanya kazi, sasa naagiza wahamishwe wapeleke Tabora na wale wa Tabora waje hapa makao makuu wapige kazi kwa kuwa mliwaleta na wakapiga kazi na tija ikaonekana, msitaka tuonekane ni wizara ya kushughulikiana, nanyi msitushughulikie," alisema Biteko.

Aidha, aliitaka tume kujiangalia maana wamepata ugonjwa mpya wa kutaka kufanya kazi mpaka walipwe posho, utaratibu wanaoutumia kudai haufai na wakitaka kuutumia wakautafutie mahali pengine na si Wizara ya Madini.

Biteko aliagiza mchakato wa kuhamisha watumishi hao wanne ambao wanastahili kuhamishiwa makao makuu ya tume Dodoma kuwa umekamilika ifikapo Desemba 9, mwaka huu mchakato huo uwe umekamilika.

Pia alimwagiza Katibu Mtendaji wa Tume, Prof. Shukrani Manya, kufanya upya mapitio ya wakuu wa idara kwa lengo la kuimarisha utendaji wa tume hiyo.

Biteko aliwataka waajiriwa wapya kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria, taratibu na kutenda haki kwa kuepuka vitendo vya rushwa ukizingatia kuwa watu wanaokwenda kuwahudumia wanamaneno mengi na majungu hivyo wasipokuwa makini watawaharibia kazi.

Aliwataka kujifunza kupitia sheria ya madini kuisoma kwa makini na kuifahamu vyema.

Biteko alitoa onyo kwa maofisa wa madini wa kanda wenye tabia ya kutegesheana kusaini madokezo jambo ambalo linachelewesha, ambapo amemwagiza katibu mkuu kufikisha taarifa kwa RMO wa aina hiyo ambaye hakutaka kumtaja jina lake, kwamba hiyo ni nafasi ya mwisho asirudie.

Prof. Manyama alisema, wamepokea watumishi wapya 116, ambao watapangiwa vituo vya kazi baada ya mafunzo hayo.

Habari Kubwa