Waliotafuna mamilioni ya Naibu Spika ‘wayatapika’

03Dec 2018
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Waliotafuna mamilioni ya Naibu Spika ‘wayatapika’

WALIOKUWA viongozi wa Soko la Sido jijini Mbeya ambao walikuwa wanatuhumiwa kutafuna fedha milioni 10 zilizokuwa zimetolewa na Naibu Spika, Dk. Tulia Akson, kama pole kwa waathirika baada ya soko hilo kuteketea kwa moto, wamezitapika katika mazingira yenye utata.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila

Oktoba 24, mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, alifanya mkutano na wafanyabiashara hao ambapo walilalamika kuwa fedha hizo hazijulikani ziliko na alipowaita viongozi hao kutoa ufafanuzi walitokomea.

Hali hiyo ilimfanya Chalamila kuingiwa na wasiwasi kuwa walikuwa wamezitafuna, ndipo akaagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwasweka ndani mpaka waeleze walikopeleka fedha hizo jambo ambalo lilitekelezwa.

Akitoa ufafanuzi wa urejeshaji wa fedha hizo juzi katika soko hilo, Chalamila alisema viongozi hao wamesharejesha fedha hizo, lakini katika mazingira ya shari na ambayo hayaeleweki mpaka sasa, lakini akasisitiza kuwa zipo katika mikono salama.

Alisema awali kabla hawajatiwa nguvuni, viongozi hao waliandika barua kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, na mawaziri wote wakidai kuwa kiongozi huyo anawaonea hawajatafuna fedha, lakini waliandika wakiwa mafichoni wameyakimbia makazi yao.

Alisema baadaye waliandika barua kuwa wanataka kurejesha fedha hizo kwa kumpelekea Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na na Rushwa (Takukuru) mkoa na kwamba alimkataza kiongozi huyo asiipokee mpaka wamkabidhi yeye mwenyewe.

“Nilimwambia Mkuu wa Takukuru kwamba kama fedha hiyo ni rushwa basi ipokee, lakini kama sio rushwa waache wanikabidhi mwenyewe, hawakufanya hivyo mpaka walipotiwa nguvuni ambapo waliziingiza kwenye akaunti ya Katibu Tawala wa mkoa wetu,” alisema.

“Tulipowahoji nani aliwapa akaunti ya Katibu Tawala hawakusema, lakini tulichojali ni kurejeshwa kwa fedha hizo, lakini kwa mujibu wa sheria, Katibu Tawala haruhusiwi kutumia fedha yoyote kwenye akaunti hiyo mpaka zipitie hazina, hivyo taratibu zitafuatwa,” alisema Chalamila.

Hata hivyo pamoja na kwamba aliagiza viongozi hao wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti, Charles Syonga na Katibu wake, Alanus Ngogo, wawepo kwenye mkutano huo ili watoe ufafanuzi lakini hawakuonekana na alipowataka wajitokeze, hakuna aliyejitokeza.

Chalamila aliwataka wafanyabiashara hao kuwa waaminifu, ili kuepuka migogoro isiyokuwa ya lazima huku akiwataka waendelee kulipa kodi ya serikali.

Katika hatua nyingine, Chalamila aliwapa siku saba wafanyabiashara wadogo wadogo waliojenga vibanda vya mbao kuzunguka Soko la Kimataifa la Mwanjelwa, kuondoa vibanda hivyo, ili kulipa hadhi soko hilo ambalo ufanisi wake ni mdogo.

Vilevile, aliwapa siku saba wafanyabiashara wanaouzia bidhaa zao katika eneo la stendi ya Kabwe na wanaouzia kwenye maeneo ya hifadhi za barabara waondoke na kwenda katika Soko la Nanenane au kwenye masoko mengine rasmi.

Aliwataka kuondoa biashara hizo kabla ya Ijumaa saa 10:00 jioni wiki hii na kwamba kwa ambaye hatakuwa ameondoa biashara hiyo asilalamike kwa kile kitakachotokea.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika, alisema wafanyabiashara waliojenga vibanda vya muda kuzunguka Soko la Mwanjelwa na wenye meza katika stendi ya Kabwe, waliwekwa kwa muda na kwamba muda wao uliisha Novemba 30, mwaka huu.

 

 

 

 

Habari Kubwa