Waliovamia viwanda waamriwa kubomoa

06Dec 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Waliovamia viwanda waamriwa kubomoa

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, amewataka wananchi wote wanaodaiwa kuvamia eneo la viwanda na kujenga makazi yao katika Mtaa wa Gombe Kusini Kata ya Itezi jijini Mbeya kuvunja nyumba zao kabla hawajachukuliwa hatua.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila (katikati), akiwa na baadhi ya maofisa wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, wakikagua maeneo ya Ngombe Kusini, katika Kata ya Itezi, juzi, yanayodaiwa kuwa yalitengwa kwa ajili ya viwanda, lakini yamevamiwa na watu waliojenga nyumba za makazi. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, William Ntinika. PICHA: NEBART MSOKWA

Chalamila alitoa agizo hilo juzi alipotembelea eneo hilo pamoja na baadhi ya viwanda vilivyopo katika eneo hilo ambapo aliambiwa na maofisa ardhi na mipango miji wa Jiji hilo kuwa baadhi ya wananchi hao ni wavamizi na wamejenga makazi ya kudumu.

Alisema baadhi ya maeneo hayo yameanza kuendelezwa na wenye viwanda, lakini wengine wanashindwa kwa sababu ya uwepo wa nyumba hizo.

Alisema baadhi ya watu hao wanatumia njia za kijanja kwenda mahakamani kwa ajili ya kuikwamisha serikali kutekeleza mipango yake na kwa kutumia baadhi ya wanasheria, hivyo akawatahadharisha kuacha tabia hiyo mara moja.

“Hatuko tayari kuingilia mahakama ila tuko tayari kuendelea na kazi zetu kama ambavyo mihimili mingine inaendelea na kazi zao, kwa hiyo wale wote waliovamia eneo lenye hati miliki kwa ajili ya viwanda, waanze kutupisha wenyewe kuanzia leo,” alisema Chalamila.

Alisema eneo hilo haliwezi kutolewa hati kutokana na kuwapo kwa hati nyingine ambayo ni maalumu kwa ajili ya viwanda, hivyo alisema watu hao hawana haki ya kukaa mahali hapo.

Akitoa taarifa ya eneo hilo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Jiji la Mbeya, Peter Msilanga, alisema eneo hilo lilipimwa miaka ya 1980 na lilitengwa kwa ajili ya viwanda lakini limevamiwa.

Alisema eneo hilo lipa katika Kitalu namba BB Uyole, na kwamba wananchi waliojenga nyumba zao kwenye eneo hilo hawana vibali vilivyotolewa na serikali na hivyo ni wavamizi.

Alisema idadi ya nyumba hizo ni kubwa, na baadhi zipo kwenye maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupitisha barabara na hivyo kulifanya eneo hilo kutokuwa rafiki kwa wawekezaji wa viwanda ambao wanataka kuwekeza.

“Watu hao wanawazuia wawekezaji kuendeleza maeneo yao kitu ambacho sasa hata sisi tunapata shida, idadi kamili ya nyumba hizo bado mpaka tutakapozihesabu,” alisema Msilanga.

Hata hivyo baadhi ya wananchi waliojenga nyuma zao kwenye eneo hilo walidai wana vibali vilivyotolewa na Idara ya Ardhi ya Jiji la Mbeya na hivyo wanashangaa kuambiwa kuwa ni wavamizi.

Mmoja wa wananchi hao ambaye hakutaka kutaja jina lake, alisema walinunua maeneo hayo kutoka kwa wenyeji waliokuwa wanayamiliki kama mashamba na wakalipia asilimia za mapato serikalini.

Alisema pamoja na kwamba wanadaiwa kuwa ni wavamizi, lakini wanalipa kodi za nyumba ambazo zinakusanywa kila mwaka na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Habari Kubwa