Walipakodi sasa kushindanishwa

22Jul 2021
Shaban Njia
Kahama
Nipashe
Walipakodi sasa kushindanishwa

SERIKALI wilayani Kahama mkoani Shinyanga imeitaka Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa maalumu wa kikodi wa Kahama kuwashindanisha walipakodi wakubwa na wadogo ili kuwajua watu wanaojitoa katika nchi hii kwa kulipa kodi bila usumbufu.

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Festo Kiswaga, aliyabainisha hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari na kuyatambulisha maonyesho ya biashara na uwekezaji yanayotarajia kufanyika mjini Kahama kuanzia Julai 30 hadi Agosti 8, mwaka huu.
 
Kiswaga alisema wilaya hiyo ni moja kati ya wilaya zinazoongoza kwa kulipa kodi nchini, hivyo katika maonyesho hayo makubwa wanatarajia kuwatambua wafanyabiashara hao kwa kuwashindanisha na kuwapatia vyeti watakaoshinda.
 
Aidha alisema, Kahama lazima iwe na chombo cha wafanyabiashara wenye nguvu na watatambulika kwa kuona ushiriki wao katika suala zima la ulipaji wa kodi na hiyo ndio heshima kubwa kwao ambayo itaondoa malalamiko ya kufungiwa biashara zao na mamlaka.
 
Alisema Kahama ni soko kubwa la nchi za jirani za Rwanda, Burundi, Kongo na Rwanda, na kwamba anataka kuona Manispaa ya Kahama inakuwa jiji hapo baadaye, kwa sababu kuna wanunuzi wakubwa kutoka nchi hizo wanaonunua mahindi, mchele, karanga, madini, tumbaku na mazao mengine.
 

Habari Kubwa