Walipwa fidi kupisha mradi umeme jua

15Feb 2020
Godfrey Mushi
Same
Nipashe
Walipwa fidi kupisha mradi umeme jua

WANANCHI wa vijiji vya Kisima na Kandoto katika Wilaya ya Same, wameanza kulipwa fidia ya mali na mazao ili kupisha ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa jua.

Taarifa iliyopatikana jana na kuthibitishwa na Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Kilimanjaro, Mhandisi Mahawa Makaka, ineleza kuwa wananchi hao wanalazimika kuondoka sasa katika eneo lenye ukubwa wa ekari 100 ambalo tayari limesanifiwa kupisha ujenzi huo.

Serikali imeanza kulipa fidia hiyo, ikiwa imepita miaka minne tangu ilipofanyika tathimini na uthaminishaji wa mali.

“Tumetenga kiasi cha Sh. bilioni 3.5 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi hawa wa Kisima na Kandoto. Katika awamu ya kwanza tutalipa Sh. bilioni 1.99 kwa wananchi 203,” alisema Mhandisi Mkaka.

Baadhi ya wananchi wa vijiji hivyo, wakizungumza baada ya maofisa wa Tanesco kufika katika mkazi yao waliishukuru Wizara ya Nishati kwa kuharakisha malipo hayo ya fidia na kuonyesha dhamira ya kuanzisha mradi wa umeme jua utakaozalisha megawati 150 ambazo zitaingizwa katika gridi ya taifa.

Fidia hiyo inalipwa kwa wakati mwafaka, kipindi ambacho serikali imenuia kuzalisha umeme wa kutosha kwa kutumia gesi asilia ili kukabiliana na upungufu unaojitokeza nchini.

Kwa mujibu wa Mhandisi Mkaka, mitambo mipya na ya kisasa itafungwa wakati wowote kuanzia sasa katika Wilaya ya Same.

Tanesco inafikia hatua hiyo, baada ya uzalishaji wa nishati ya umeme ukiwa unabadilika kadri teknolojia zinavyobuniwa na kukua, pamoja na kwamba Tanzania kwa miaka yote imekuwa ikitegemeza zaidi teknolojia kongwe ya umeme wa maji.

Mitambo ya umeme wa maji kwa kawaida huzalisha asilimia 35 ya mahitaji yote ya umeme Tanzania, huku gesi asilia na mafuta hujazia asilimia zinazobaki.

Habari Kubwa