Wamachinga rasmi TRA kulipa kodi

28Mar 2018
Beatrice Shayo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wamachinga rasmi TRA kulipa kodi

WAFANYABIASHARA wadogo wasiokuwa kwenye sekta rasmi wameanza kupatiwa vitambulisho maalum ili kuingizwa kwenye mfumo wa ulipaji wa kodi.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere, wakati wa uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga,  alisema kwa wafanyabiashara hao watakuwa wanalipia Sh. 10,000 kama gharama ya kuchangia kitambulisho hicho.

Alisema utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara hao unatokana na marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Kodi ya  mwaka 2015 yaliyofanywa na Bunge la bajeti la mwaka 2017/18 ambapo moja ya marekebisho hayo ni kuwatambua na kuwapatia vitambulisho maalumu wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi.

”Zoezi hili linatekelezwa na TRA kwa kushirikiana na Mamlaka ya Vitambulisho cha Taifa (Nida), Tamisemi, Wakala wa Usajili, Ufilisu na Udhamini (Rita) pamoja na Idara ya Uhamiaji,” alisema.

Kichere alisema TRA kwa kushirikiana na wadau hao ilianza kutekeleza jukumu hilo kwa kuutambua umoja wa wamachinga wa Kariakoo jijini Dar es Salaam na kuwapatia vitambulisho vya taifa na namba ya  utambulisho wa mlipakodi (TIN).

Alisema kundi hilo ni miongoni mwa waliopatiwa vitambulisho maalumu vya wafanyabiashara wadogo kama ishara ya uzinduzi wa utoaji wa vitambulisho hivyo.

Kwa mujibu wa Kichere, wameanza kutoa vitambulisho hivyo kwa wilaya ya Ilala na baada ya hapo watakwenda mikoani ili wafanyabiashara wote ambao hawapo kwenye sekta rasmi waweze kupatiwa vitambulisho kwa gharama hiyo.

Aidha, alisema ili wafanyabiashara wadogo waweze kupata vitambulisho hivyo, watatakiwa kujiunga katika vikundi vinavyotambulika kisheria na serikali, kuwa na kitambulisho cha taifa, kuwa na TIN ya kikundi alichokiunga nacho na kuchangia Sh. 10,000.

Kichere alisema vitambulisho maalum kwa wafanyabiashara wadogo walio kwenye sekta isiyo rasmi vitadumu kwa miaka mitatu.

Aidha, alisema serikali inawatambua wafanyabiashara wadogo, hivyo ni muhimu wakajiunga kwenye vikundi ili waweze kupatiwa vitambulisho maalum.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, aliishukurua TRA kwa  kutekeleza ahadi ya utoaji wa vitambulisho kwa wafanyabiashara wadogo ambao hawapo katika sekta isiyo rasmi.

Alisema serikali na wamachinga wamekuwa wakisubiri utekelezaji wa mpango huo tangu mwaka 2016.

Mjema pia alimshukuru Rais John Magufuli kwa kuwajali wafanyabiashara wadogo na kwamba mkakati wao ni kuhakikisha wafanyabiashara hao wanajulikana na kupatiwa vitambulisho.  

 

 

 

Habari Kubwa