Wambana bosi TRL mil. 600/-

03Aug 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es salaam
Nipashe
Wambana bosi TRL mil. 600/-

WAFANYAKAZI zaidi ya 500 wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), wamemlalamikia Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Masanja Kadogosa, kwa kutowalipa Sh. milioni 600 yakiwa ni makato kutoka Chama cha Ushirika cha Akiba na Mikopo cha Tanga District Railways Savings and Credit Society Ltd.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Masanja Kadogosa.

Fedha hizo ni makato ya mishahara waliyokuwa wanakatwa wafanyakazi wa TRL na wastaafu kwa miezi 10 na kutoingizwa katika Ushirika huo.

Wamemwomba Rais John Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuingilia kati ili wapate fedha hizo.

Akizungumza na Nipashe kwa niaba ya wenzake, Meneja wa ushirika huo, Ambilikile Mwambuluma, alisema tangu Septemba 2015 chama hicho kimekumbwa na matatizo ya kutolipwa fedha za makato ya wanachama wake ikiwa ni akiba, mikopo na riba kutoka kwa mwajiri ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa TRL.

“Mpaka kufikia Juni 30, mwaka huu tunamdai Mkurugenzi wa TRL Sh. milioni 614.61 zikiwa ni fedha za makusanyo ya marejesho ya miezi 10,” alisema Ambilikile.

Alisema wanawaomba viongozi wa juu wa Serikali kusikia kilio chao na kuwasaidia kupata fedha hizo ili kukinusuru chama ambacho kinawasaidia kutatua baadhi ya matatizo ya kijamii.

Alisema Februari mwaka huu walimwandikia barua Mkurugenzi Mkuu TRL kuomba kulipwa Sh. milioni 200 kwa ajili ya mkutano mkuu, lakini walipewa Sh. milioni 101.64.

Alisema wameshamwandikia barua tano Mkurugenzi Mkuu wa TRL za kuomba fedha hizo, lakini walijibiwa barua mbili tu zilizokuwa na ahadi zisizotekelezwa.

Alieleza Ushirika ulimtuma Mwenyekiti na Meneja wa ushirika jijini Dar es Salaam kuonana na Mkurugenzi Mtendaji, lakini walipewa ahadi ya kulipwa fedha hizo ndani ya mwezi mmoja.

“Mpaka sasa ni mwezi mmoja umepita tangu tulipopewa ahadi ya kulipwa na hatujalipwa chochote, inasikitisha sana wanatuahidi, lakini hakuna utekelezaji, tukiuliza sababu za kutolipwa Mkurugenzi anasema anazitumia kutengeneza njia ya reli na madaraja,” alisema Ambilikile.

Nipashe lilimtafuta Kadogosa bila ya mafanikio, lakini Msemaji wa TRL, Medladjy Maez, alikiri kulifahamu suala hilo na kusema limeshamfikia Mkurugenzi Mtendaji wa TRL.

Alisema kupitia mkutano wa wafanyakazi uliofanyika Julai 28, mwaka huu, waliwasilisha malalamiko mengi likiwamo la madai hayo ya fedha.

“Tunawashangaa hao walioongea na waandishi, wakati suala hili lilijadiliwa katika mkutano na madai yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi, na yanashughulikiwa,” alisema Maez na kuongeza, Mkurugenzi Mtendaji hakuwapo ofisini kwa muda, lakini amesharudi na atalifanyia kazi.

Habari Kubwa