Wamiliki migodi tanzanite watakiwa kulipa leseni uchimbaji

14Jan 2022
Jaliwason Jasson
Simanjiro
Nipashe
Wamiliki migodi tanzanite watakiwa kulipa leseni uchimbaji

WAMILIKI wa migodi ya madini ya tanzanite katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, wametakiwa kulipia leseni wanazozimiliki ili waendelee kufanya kazi zao kwa uhuru.

Zaidi ya migodi 2,000 ya madini ya tanzanite imekatiwa leseni ya uchimbaji ila iliyopo hai na inayofanyiwa kazi ni migodi 300 pekee.

Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, Fabian Mshai, aliyasema hayo wakati akizungumza na samiliki na mameneja wachimbaji wa madini ya tanzanite wa Mji mdogo wa Mirerani.

Mshai alisema wamiliki wa migodi ya madini ya tanzanite, wanaodaiwa fedha za leseni zao wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa kulipa ili kuondokana na kero ya kufuatwa kila wakati.

Alisema leseni zisipofanyiwa kazi zinasababisha madeni kwani wanapoomba wanapaswa kuziendeleza kwa kuhakikisha zinafanya kazi.

"Hivi sasa kuna madeni mengi ya fedha za leseni takribani Sh. milioni 300, hivyo wale wote wanaodaiwa wafike ofisini ili walipe na kuendeleza sekta ya madini," alisema Mshai.

Katibu wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Manyara (MAREMA), Tariq Kibwe, alisema suala la wachimbaji kulipia leseni zao halikwepeki, hivyo watekeleze wajibu wao.

Ofisa Mkaguzi Migodi, Castro Maduwa, alisema wachimbaji wanaponunua zana za milipuko wanapaswa kuwa na vibali ili kuepusha ajali zisizokuwa za lazima.

Mwenyekiti wa wachimbaji wa madini ya tanzanite, Money Yusuf alisema mchimbaji anapaswa kuzingatia agizo la kuwa na kibali cha milipuko kwani wanaweza kukamatwa na serikali wasipokuwa na vibali hivyo.

Habari Kubwa