Wamwagiwa mikopo ya mil. 40/-

16Apr 2019
Zanura Mollel
Longido
Nipashe
Wamwagiwa mikopo ya mil. 40/-

HALMASHAURI ya Wilaya ya Longido imetoa Sh. milioni 40 ambazo ni sehemu ya makusanyo ya mapato ya ndani kwa vikundi 14 kutoka kata 10 kati ya 18.

Akikabidhi hundi kwa vikundi hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri, Nestory Dagharo, ambaye ni Ofisa Mifugo katika halmashauri hiyo, alisema fedha hizo ni asilimia 10 ya agizo la serikali kutolewa katika mapato ya ndani na kuwezesha vikundi maalumu.

Aliwataka walengwa wa fedha hizo kuzitumia katika kile walichokiombea na kurejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kusaidia vikundi vingine vyenye uhitaji wa mikopo hiyo.

"Vikundi ni vingi ndani ya wilaya na wameomba mikopo, ninyi mmebahatika, kafanyieni kazi na mkumbuke kurejesha," alisema Dagharo.

Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Grace Mghase, alisema vikundi vilivyopewa mikopo ni 14, ambavyo sita ni vya wanawake, vitano vya vijana na vitatu vya watu wenye ulemavu.

Alieleza kwa mwaka wa fedha 2018/19 halmashauri imetoa jumla Sh. 92,630,000 hadi kufikia robo ya pili.
"Robo ya kwanza na ya pili tumetoa Sh. 92,630,000 na sasa robo ya tatu ya mwaka tunatoa Sh. milioni 40," alisema Grace.

Alieleza mchanganuo wa fedha hizo katika makundi ni vikundi sita vya wanawake watapewa Sh. milioni 18.5, za vijana watapatiwa Sh. milioni 14 na vikundi vitatu vya walemavu watapewa Sh. milioni 8.

Baraka Laize, mwenye ulemavu ambaye mnufaika wa mikopo hiyo alisema watatumia fedha hizo kununua mifugo na kunenepesha ili wajikwamue kiuchumi.

Alidai miaka ya nyuma walemavu walikuwa hawatambuliki na kuonekana ni watu ambao hawawezi, lakini kwa sasa anaona mabadiliko makubwa kwa serikali yao kuwajali.

Alieleza jamii ya kifugaji haina utaratibu wa kuwathamini watu wenye ulemavu, hivyo, wengi wao huishia kufungiwa ndani na kunyimwa haki zao za msingi.

"Sisi tunaishukuru halmashauri yetu kwa kutoa asilimia 2 ya walemavu, lakini pia tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge," alisema.

Habari Kubwa