Wamwomba Rais maeneo ya biashara stendi mpya

02Jun 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Wamwomba Rais maeneo ya biashara stendi mpya

WAFANYABIASHARA ndogo na mamalishe zaidi ya 100 katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wamemwomba Rais John Magufuli, kuwasaidia kupata nafasi ya kufanyia biashara zao, baada ya halmashauri kushindwa kuwapa kipaumbele kwenye ugawaji wa maeneo katika stendi mpya ya mabasi.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Patrobas Katambi:PICHA NA MTANDAO

Akizungumza jana na waandishi wa habari, mmoja wa wafanyabiashara ambao kwa sasa wapo katika stendi ya muda ya Nanenane, Emanuel Kamboya, alisema kuwa waliahidia na halmashauri hiyo kuwa wao ndiyo watakaopewa kipaumbele baada ya stendi hiyo kukamilika.

Kamboya, alisema awali walihamishwa kutoka eneo iliyokuwa stendi kuu ya mabasi eneo la mjini ambako Shirika la Reli nchini (TRC), ndiyo walikuwa wamiliki na kuondoa kupisha Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

“Awali tulikuwa tukifanya biashara katika stendi ya zamani ya mkoa ya kule mjini ambako tulivunjiwa vibanda vyetu baada ya TRC, kulichukua eneo lao na jiji wakatuamuru wote tuje huku Nanenane, katika stendi ya muda na baada ya kukamilika kwa stendi mpya sisi ndiyo tuliahidiwa kupewa kipaumbele,” alisema Kamboya.

Alisema pamoja na kuahidiwa kuwa watapewa kipaumbele cha kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara, hali imekuwa tofauti kwa kuwa waliopatiwa maeneo katika stendi mpya ni watu wengine tofauti na wao.

“Waliopewa ni watu tofauti kabisa na sisi ambao tulikuwa tunafanya biashara katika stendi ya kwanza iliyovunjwa, tumetafuta msaada katika maeneo mbalimbali kwa viongozi wetu tumeshindwa, hivyo sasa tunamwomba Rais Magufuli, atusaidie na sisi kupata maeneo kwa kuwa kuanzia leo (jana), stendi mpya inaanza kutumika rasmi,” alisema.

Naye Tausi Maulidi, alisema lengo la kumwomba Rais Magufuli kuwasaidia ni kutokana na kukosa msaada kwa viongozi waliowalilia kilio chao.

“Sisi hapa tulipo hatuna kitu kingine cha kukitegemea kupata riziki yetu ya kila siku, lakini tuna mikopo ya kuendesha biashara zetu, tukikosa nafasi ya maeneo ya kufanya biashara tutakosa namna ya kuishi na familia zetu,” alisema Maulidi.

Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, alikiri wafanyabiashara hao kuahidiwa na halmashauri kuwa ndiyo wangepewa kipaumbele.

Katambi alisema, kutokana na janga la corona, jiji liliamua kutumia mfumo wa kuomba maeneo kwa njia ya mtandao hali ambayo ili mlazimu kila mtu kuomba eneo kwa usawa bila kujali nani alikuwapo awali.

“Kweli hawa wafanyabiashara, waliahidiwa na jiji kupatiwa kipaumbele, lakini mfumo uliotumika sasa ulihusisha watu wote na wao pia walipaswa kuomba kama wengine, lakini nimeshaongea na watu wa jiji wakutane nao ili kuwaelimisha,” alisema Katambi.

Habari Kubwa