Wanachama wa kuweka na kukopa wahimizwa kujiunga bima ya afya

12Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Babati
Nipashe
Wanachama wa kuweka na kukopa wahimizwa kujiunga bima ya afya

CHAMA cha kuweka na kukopa cha Mabadiliko Saccos cha mjini Babati kimetoa mkopo wa pikipiki 15 zenye thamani ya Sh. milioni 33 na cherehani moja ya Sh. 300,000 ili kuwanyanyua kiuchumi wanachama wake.

Mkuu wa Wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu, akizungumza wakati wa kukabidhi pikipiki hizo juzi, aliwataka wanachama hao wajiunge na mfuko wa afya ya jamii.

Alisema vijana hao watakapokuwa na kadi hiyo ya afya ya jamii, wataweza kupata matibabu pindi wakiugua.

Alisema kujiunga na mfuko wa afya ya jamii ni jambo zuri kwani watakuwa wanachama waliopo kwenye bima na wenye uhakika wa matibabu endapo wakiugua.

"Pia muwe mabalozi wazuri kwa wengine ambao hawajajiunga na mfuko huo muwaeleze waweze kujiunga na kufaidika na huduma hiyo ya kupata matibabu wanapougua," alisema.

Mratibu wa Mabadiliko Saccos, Hussein Abrima, alisema ilisajiliwa Novemba 15, mwaka 2017.

Abrima alisema chama chao kina wanachama 96 hai waliopo kwenye mitaa mbalimbali ya mjini Babati, ambao walikuwa kwenye vikundi vingine vya ujasiriamali.

Mbunge wa Jimbo la Babati mjini, Pauline Gekul, aliwapongeza wote waliopata mkopo huo na kwa kuwataka watumie mikopo hiyo kwa malengo yaliyopaswa.

Alisema vijana hao wakitumia mikopo hiyo vizuri watajinyanyua kiuchumi na kusababisha wengine pia wachukue mikopo kwa mzunguko huo.

Mmoja kati ya waliopata mkopo wa pikipiki, Mohamed Hussein, ambaye ni dereva wa bodaboda alisema hivi sasa amepata faida ya kujiunga kwenye vikundi vya ujasiriamali kwa kupata mkopo huo.

"Kwa sababu ya elimu ya ujasiriamali niliyonayo nitafanya kazi kwa umadhubuti kwa lengo la kurejesha mkopo na kuimiliki kabisa pikipiki hii ninayotumia kwa bodaboda," alisema.

Fundi cherehani, Sofia Nyagambe, alisema mkopo wa cherehani huo utamnufaisha kwani atarejesha mkopo huo kwa muda mfupi na kuimiliki tofauti na awali hakuwa nayo.

Habari Kubwa