Wanafunzi kilimo wapewa fursa SBL

28May 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Wanafunzi kilimo wapewa fursa SBL

WANAFUNZI wanaosomea masomo ya kilimo katika vyuo mbalimbali vinavyofundisha masomo hayo nchini, wamehakikishiwa kuendelea kupatiwa ufadhili wa masomo.

Wamepewa uhakika huo na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kwa kueleza kuwa itaendelea na programu yake ya kutoa ufadhili kwa inayojulikana kama Kilimo Viwanda Scholarship.

Hatua hii ya SBL inakuja baada ya serikali kutangaza kuwa vyuo vyote vitafunguliwa kuanzia Juni Mosi, mwaka huu  kutokana na kupungua kwa maambukizo ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu au Covid-19.

Taarifa ya jana ilisema  imeshakamilisha makubaliano na vyuo viwili zaidi kimoja cha Iringa na kingine cha Kagera ambapo jumla ya wanafunzi 20 kutoka vyuo hivyo viwili watanufaika na ufadhili huo wa masomo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mahusiano kwa Umma wa SBL John Wanayancha, vyuo viwili ambavyo ni Kaole Wazazi College of Agriculture cha Bagamoyo mkoani Pwani na Kilacha Agriculture and Livestock Training Center cha Moshi  mkoani Kilimanjaro vimeshaingia makubaliano na kampuni hiyo na  wanafunzi 20 wananufaika na ufadhili wa masomo.

Programu ya Kilimo Viwanda Scholarship inawalenga wanafunzi kutoka katika jamii za wakulima zenye vipato duni na ambazo haziwezi kuwalipia ada watoto wao. Kupitia programu hii, jumla ya wanafunzi 40 watakuwa wakinufaika na ufadhili wa masomo kila mwaka.

“Tunaamini programu hii itasaidia kuongeza wataalamu wa kilimo nchini ambao ni nguzo muhimu ya kuwasaidia wakulima kuongeza tija katika uzalishaji, hivyo kuwasaidia kuongeza kipato chao,” alisema Wanyancha.

Aliongeza kuwa programu hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo wa kuongeza kiasi cha nafaka ambacho kampuni hiyo inanunua kwa ajili ya uzalishaji wa bia ambazo ni pamoja na mahindi, shayiri na mtama. Alisema, mwaka jana ilinunua zaidi ya tani za ujazo 17,000 za nafaka kutoka kwa wakulima wa ndani sawa na asilimia 70 ya mahitaji yake yote ya malighafi kwa mwaka.

“Kampuni inalengo la kuongeza kiasi cha malighafi inayonunua kutoka kwa wakulima wa ndani hadi asilimia 85 kufikia mwaka 2020 na ndiyo maana tumeona umuhimu wa kusaidia kusomesha wataalamu wa kilimo ili wakafanye kazi ya kuboresha kilimo chetu. Kwa sasa kampuni inanunua malighafi kutoka kwenye mtandao wenye wakulima 400 nchini,” alisema.

Habari Kubwa