Wanafunzi walia ajali za bodaboda

13May 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanafunzi walia ajali za bodaboda

KATIKA kuadhimisha wiki ya Kimataifa ya Usalama Barabarani, wanafunzi wa Shule ya Msingi Bunge, wamewataka maderava wa pikipiki kuheshimu sheria za usalama barabarani.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Dunia (WHO) watoto kuanzia miaka mitano hadi 29 ndio wanaopoteza maisha kwa ajali za barabarani.

Wakizungumza na waandishi wa habari juzi jijini Dar es Salaam, katika kuadhimisha siku hiyo iliyoandaliwa na Kampuni ya Mafuta ya Puma, walisema madereva wa pikipiki hawaheshimu alama za vivuko na hata wanapokuwa wamesimama eneo la kivuko hawasimami.

Zuwena Seleman, mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Bunge, alisema wanapokuwa eneo la kivuko madereva pikipiki hukatiza bila kuangalia usalama wa watembea kwa miguu.

"Tunawaomba madereva wa pikipiki wakifika eneo la kivuko wapunguze mwendo, watii sheria za usalama barabarani na waruhusu wanafunzi tuvuke pindi wanapotuona. Wakati mwingine wakitukuta tunavuka barabara wanatutukana matusi ya kudai tunawachelewesha," alisema Nelian Edwin, mwanafunzi wa darasa la sita katika shule hiyo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mafuta ya Puma, Dominic Dhanah, alisema wameamua kuitumia siku hiyo kutoa elimu kwa madareva kuhusu kuzingatia sheria za usalama barabarani.

"Puma tumeungana na WHO kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Bunge ambao ni mabalozi wa elimu ya usalama barabarani hususani kwa Mkoa wa Dar es Salaam," alisema.

Alisema wameamua kuwatumia watoto kutoa elimu ya usalama barabarani kwa lengo la kuongeza uelewa kwa madereva hususani wa pikipiki kuhusu masuala ya usalama barabarani.

Dhanah alisema kampuni ya Puma Energy itaendelea kushirikiana na taasisi zitakazoendesha mipango mbalimbali ya usalama barabarani kwa lengo la kuhakikisha kuwa watu wanakuwa salama.

Awali Meneja Mpango wa Usalama Barabarani waWHO, Neema Swai, alisema kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Sema Usikike, Okoa Maisha' na kufafanua maadhimisho hayo huadhimishwa kila baada ya miaka miwili.

"Kila siku watoto ndio wanaotumia barabara kwenda shule na kurudi nyumbani, wasipokuwa na elimu ya kutosha tutawapoteza wengi. Mtambue, kwa mujibu wa takwimu WHO, watoto wenye umri kati ya miaka mitano hadi 29 wanapoteza maisha kwa wingi kutokana na ajali, si Malaria wala ugonjwa mwingine ni ajali," alisema Swai.

Kwa mujibu wa takwimu za WHO nchini, watu 32 wapoteza maisha katika ajali 100,000 zinazotokea, huku madereva wa pikipiki wakiongoza kwa asilimia 28 na watembea kwa miguu kwa asilimia 26.

Habari Kubwa