Wanaokiuka mikataba mashamba ya kahawa kunyang'anywa umiliki

05Jan 2017
Godfrey Mushi
SIHA
Nipashe
Wanaokiuka mikataba mashamba ya kahawa kunyang'anywa umiliki

WAWEKEZAJI wakubwa wa mashamba ya kahawa wilayani Siha wanadaiwa kushindwa kutekeleza makubaliano ya mkataba wa ufufuaji wa zao hilo kwa kubadili uwekezaji wao kwenda kwenye mazao ya muda mfupi wakisingizia mitaji midogo.

Hali hiyo inatokana na ekari 2,300 za mashamba ya vyama vya ushirika yaliyomilikishwa kwa wawekezaji hao hivi sasa kutumika kulima mboga, mahindi na maharage badala ya zao hilo.

Ofisa Ushirika wa Wilaya ya Siha, Anastazia Mahoo, aliyasema hayo juzi wakati akitoa taarifa ya hali ya ushirika kwa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa wa Kilimanjaro iliyoongozwa na mkuu wa mkoa huo, Said Mecki Sadiki.

Mkuu huyo wa mkoa huo na kamati yake walikuwa wamekwenda kutembelea mashamba hayo ili kuangalia shughuli za uzalishaji wa kahawa zinazofanywa na wawezaji wakubwa kutoka ndani na nje ya nchi.

“Nia njema ya serikali kutaka kufufua zao la kahawa katika wilaya yetu inakwama, wawekezaji waliopewa mashamba wameshindwa kutekeleza makubaliano wakidai hawana mitaji ya kutosha, lakini pia mashamba yameathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi na udongo kuwa na magadi,”alisema ofisa huyo.

Akitoa kauli ya serikali, Sadiki ambaye alionyesha kukerwa na hali hiyo, alisema wawekezaji walioshindwa kutekeleza mikataba hiyo Tanganyika mashamba hayo na kupewa wawekezaji wengine watakaoendeleza zao hilo.

“Hatuna mzaha, tutayachukua mashamba hayo na kuingia mkataba na wawekezaji wenye uwezo wa kulima kahawa na si vinginevyo. Hatuwezi kuvumilia wanaokiuka makubaliano,”alisisitiza.

Nipashe ilipowatafuta baadhi ya wawekezaji wazawa wa zao hilo katika wilaya ya Siha (majina yamehifadhiwa) ili kuzungumzia madai hayo, walikiri kushindwa kufufua zao la kahawa wakidai hali hiyo inatokana na changamoto mbalimbali ikiwamo ukame.

Habari Kubwa