Wanaokwepa kutumia EFD watangaziwa vita

12Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wanaokwepa kutumia EFD watangaziwa vita

MKUU wa Wilaya ya Kahama, Fadhil Nkurlu, ametangaza vita dhidi ya wafanyabiashara wilayani humu wanaokwepa kutumia mashine za kielektroniki (EFD).

Nkurlu amesema kitendo wanachofanya wafanyabiashara hao wanaisababishia serikali hasara na ni kinyume cha sheria.
Aliweka msimamo huo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi.

Nkurlu alisema kitendo cha wafanyabiashara kuendelea kuzikwepa kutumia mashine hizo, husababisha serikali kukosa mapato.

Alisema katika uchunguzi uliofanyika wilayani humu wa kufahamu kama mashine hizo zinatumiwa na wafanyabiashara, umebaini kuwa wapo wasiozitumia na wengine kutotoa stakabadhi kwa bidhaa wanazoziuza.

Alisema licha ya kwamba wafanyabiashara wengi wamenunua mashine hizo, lakini wengi wao hawatoi stakabadhi za kielekroniki na badala yake hutoa risiti zinazoandikwa kwa mkono.

Aidha, alisema baadhi ya wafanyabiashara hao hutumia mashine hizo kuandika fedha kidogo ya mauzo tofauti na mauzo halisia.

“Serikali imefanya utafiti na kubaini kuwa wenye mashine za EFD hawazitumii, badala yake wanatumia karatasi kumpa mteja stakabadhi na wengine hawatoi kabisa, sasa tutawashughulikia kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wilaya.

Nkurlu aliiagiza TRA wilayani humu kupita kwa wafanyabiashara ili kubaini kama wapo wasiotumia mashine hizo ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Katika kupambana na wanaokwepa kulipa mapato kwa serikali, pia Mkuu huyo wa Wilaya alisema wapo watu wamekuwa wakiuziana majengo bila kufuata sheria na kuikosesha serikali stahiki zake.

Alisema wameanza kulishughulikia na mpaka sasa wafanyabiashara watatu waliitwa na mkuu huyo wa wilaya kwa kuuziana majengo kimyakimya bila serikali kupata mapato ya asilimia 10 ya mauzo yao.

Ili kukomesha tabia hiyo, Mkuu huyo wa wilaya alitoa siku saba kwa wafanyabiashara hao ambao amewahi kuwaita ofisini kwake kwa kuuziana majengo kinyume cha sheria wawe wamewasilisha mikataba ya mauziano ya majengo hayo ili serikali ipate mapato yake la sivyo atazifunga biashara zinazofanywa na watu walionunua majengo hayo.

Habari Kubwa