Wanaovuna asali kwa kuchoma nyuki waonywa

06Dec 2019
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Wanaovuna asali kwa kuchoma nyuki waonywa

WAFUGAJI wa nyuki visiwani Zanzibar wamepigwa marufuku kuvuna asali kwa njia ya kizamani ya kuchoma moto ambayo huwateketeza.

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk. Makame Ali Ussi, picha mtandao

Naibu Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Dk. Makame Ali Ussi, alipiga marufuku hiyo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Ziwani Pemba, Suleiman Ali Makame, aliyetaka kujua hatua zinazochukuliwa na serikali kukabiliana na watu wanaovuna asali kwa kuteketeza nyuki.

Dk. Ussi alisema kitendo hicho ni uharibifu wa mazingira kwa wavunaji asali kuchoma moto nyuki wakati wakiwa katika harakati za kugema (kuvuna) asali.

Alisema matukio kama hayo athari zake kubwa zimeonekana ikiwamo baadhi ya misitu kuteketea kutokana na tabia ya wafugaji kuchoma moto wakati wakigema asali.

''Haikubaliki ni kitendo cha uharibifu wa mazingira wakati nyuki akiwa anahitajika kwa ajili ya kuzalisha asali watu wanawateketeza kwa kuwachoma moto,” alisema.

Alisema wameanza kutoa mafunzo kwa wafugaji kuhusu njia sahihi za kuvuna asali bila ya kusababisha madhara ya kuua nyuki.
Alisema jumla ya wafugaji nyuki 700 wamepatiwa elimu ambayo itawawezesha kuvuna asali kwa njia za kisasa bila ya kuharibu mazingira.

Pia alisema jumla ya vikundi 250 vimepatiwa mizinga ya kibiashara kwa ajili ya ufugaji.

''Vikundi vya wafugaji asali vingi tumevipatia mafunzo juu ya kuvuna asali kwa kuzingatia mazingira na uhifadhi wake...sioni sababu ya kuchoma nyuki wakati wa kuvuna asali,” alisema.

Dk. Ussi aliwajulisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwamba shughuli za kufuga kwa ajili ya kuzalisha asali imeanza kuleta matunda mazuri kwa wananchi wa Unguja na Pemba ikiwamo kujitokeza vikundi vingi kwa ajili ya kazi hizo.

Habari Kubwa