Wanawake kuonyeshwa fursa za utalii

25Feb 2021
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake kuonyeshwa fursa za utalii

BODI ya Utalii Tanzania(TTB), inatarajia kuwakutanisha wanawake kutoka katika mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza  kwa ajili ya kuwaelimisha namna ya kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Devotha Mdachi, alisema tukio hilo litafanyika Machi 8, mwaka huu katika maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani, na kwamba lengo ni kuthamini mchango wao katika kukuza utalii.

Alisema ipo haja kwa wanawake kuhakikisha wanachangamkia fursa  mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo ikiwamo kumiliki makampuni makubwa yanayojihusisha na shughuli hizo za utalii.

“Wanawake ni kundi muhimu katika kuchangia maendeleo katika sekta hii ya utalii, tumekuwa tukishuhudia wakifanya shughuli mbalimbali katika maeneo mengi ya utalii, tunataka tuwakutanishe kuwapatia mbinu zaidi za kuteka kila fursa iliyopo katika sekta hii,” alisema Mdachi.

“Hatutaki waishie tu katika kufanya shughuli ndogo, tunataka pia wafanye shughuli kubwa kama kumiliki makampuni yao wasiseme ni kazi zinazotakiwa kufanywa na wanaume peke yao.”

Alisema katika madhimisho hayo, kutakuwa na kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii na kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

“Tunatambua thamani ya mwanamke katika kuchangia kukuza uchumi wa taifa, tunamtambua kwamba ni jeshi kubwa, tunamuenzi kwa kuitumia siku hii kutambua mchango wake katika sekta hii ya utalii,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TABWA), Noreen Mawalla, alisema watahakikisha wanawawezesha wanawake hao katika kuchangamkia kila fursa iliyopo katika sekta ya utalii.

“Zamani kulikuwa na kasumba kwamba zipo baadhi ya kazi ambazo wanawake hawawezi kufanya, tunataka dhana hii ifutike, tutachangamkia fursa yoyote inayojitokeza mbele yetu ilmradi isiwe ya kuvunja sheria, na tunataka kufanya kazi kwa bidii zote ili kujenga uchumi wetu na wa nchi yetu,” alisema Mawalla.

Habari Kubwa