Wanawake waaswa kuchangamkia mikopo ya halmashauri

16Mar 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Wanawake waaswa kuchangamkia mikopo ya halmashauri

WANAWAKE katika Halmashauri ya Arusha, wametakiwa kubadili fikra za kuwa tegemezi kwa waume zao na badala yake watumie fursa ya kukopa mikopo ya halmashauri inayotolewa kwa ajili yao ili wajikwamue kiuchumi.

Wito huo ulitolewa jana jijini hapa na Ofisa Maendeleo ya Jamii, Mkoa wa Arusha, Irene Materu, wakati akizungumza na vikundi vya wanawake wajasiriamali wa halmashauri hiyo, kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari ya Enaboishu wilayani Arumeru mkoani hapo.

Alisema wanawake wanatakiwa kutumia fursa zinazotolewa na serikali na wadau mbalimbali, ikiwamo mikopo inayotozwa asilimia nne inayotolewa na halmashauri kwa ajili ya wanawake, ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali.

“Ufike wakati sasa wanawake tukatae kuwa tegemezi, tujikwamue kiuchumi kwa ajili ya kutunza na kuendeleza familia zetu kwa kupata lishe bora kupitia fursa mbalimbali zinazowalenga wanawake,” alisema.

Aidha, alisema wanawake ni nguzo kuu katika jamii, lakini pia ni msingi mkubwa wa maendeleo, hivyo kuna kila sababu kwao kubadilisha mtazamo na kuwa na fikra chanya ili waweze kufikia malengo waliyojipangia katika kujiletea maendeleo.

Irene alitumia fursa hiyo kulaani vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike na kuwataka wanawake kuwa jasiri kwa kupinga vitendo vya ukatili kwenye familia zao na jamii inayowazunguka, ikiwa ni pamoja na kuwafichua wanaowapa mimba wanafunzi wa kike ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.

"Tusikubali kudhalilishwa, tuanze sisi wenyewe kukemea vitendo vya ukatili vinavyodhalilisha utu wa mwanamke, pia tuwafichue wanaowapa mimba watoto wetu wa kike wakiwa na umri mdogo na kuwakatisha masomo ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa serikali ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu hao,” alisema.

Aliwataka wanawake hao kutumia kikamilifu majukwaa ya wanawake katika maeneo yao kwa kujadili changamoto zinazowakabili,
lakini pia kubadilishana uzoefu wa miradi ya ujasiriamali wanaoufanya pamoja na kupeana fursa za kufikia malengo ya kupata mafanikio.

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Arusha (UWT), Yasimin Bachu, alisema wanawake wanatakiwa kutunza familia zao, ili taifa liweze kuwa na wananchi wachapa kazi kutokana na lishe bora.

Yasmin ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum, aliwataka wanawake kupima afya zao kila mara, ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi ili kuepuka maradhi ambayo yanakwamisha na kurudisha nyuma gurudumu la maendeleo katika taifa letu.

Awali Ofisa Maendeleo ya Jamii na Jinsia, Halmashauri ya Arusha, Getrude Darema, alisema jumla ya wanawake wajasiriamali 395 kwenye
vikundi 45, wamewezeshwa na halmashauri hiyo, kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba yenye thamani ya Sh. milioni 243, fedha zinazotokana na asilimia nne za mapato ya ndani kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019.

Alisema licha ya vikundi hivyo, halmashauri inatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya Sh. milioni 80 kwa vikundi vingine vinane
leo na kuwahimiza wanawake kutumia vyema fursa hiyo kwa kuanzisha miradi ya kibiashara itakayowawezesha kujikwamua
kiuchumi na si vinginevyo.

Habari Kubwa