Wanawake wafundwa kuhusu uwekezaji

08Feb 2016
Nipashe
Wanawake wafundwa kuhusu uwekezaji

WANAWAKE nchini wametakiwa kuwa na utaratibu wa kumiliki ardhi, kujiwekea akiba, kujiunga na bima mbalimbali pamoja na kuandika mirathi ili kurahisisha maisha ya uzeeni.

Wito huo, ulitolewa na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake, Magreth Chacha, wakati akizungumza na wanachama wa Royal Women Group katika sherehe yao ya kuukaribisha mwaka 2016, iliyofanyika juzi Msasani jijini Dar es Salaam.

Alisema ni wakati wa wanawake kujitambua na kuamini kuwa wanaweza kumiliki vitu vikubwa kama meli, ndege na mambo mengine badala ya kuendelea kuwa watumwa wa kutojiamini.

Aliwataka wanawake kutambua thamani yao na nafasi walizonazo katika jamii ili kufikia malengo makubwa ikiwa ni pamoja na kushika kubwa kama kuwa wakurugenzi na wamiliki wa kampuni.

“Nachotaka kuwaasa ni kuwa wanawake ni jeshi kubwa, tunaweza bila hata kushikwa mkono. Tujitahidi kumiliki ardhi hiyo ni hazina inayoweza kukusaidia uzeeni, kuandika miradhi juu ya mali unazomiliki ili kuwarahisishia kazi watoto na ndugu, pia jiangalieni kama watu mnaoweza kumiliki mali nyingi na siyo kuwa wanawake wa kujiwazia mambo madogo,” alisema.

Naye Mkurugenzi na Mmiliki wa Maznat Salon, Maza Sinare Mchome, aliwataka wanawake kujiamini na kusimamia kile wanachokiamini ili kufikia malengo yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jumla Professional Approach Group, Modesta Mahiga, aliwataka wanawake kujiwekea malengo makubwa bila kuangalia mazingira na watu wanaomzunguka ikiwa ni pamoja na kuwania nafasi kubwa za uongozi.

Akizungumzia mafanikio ya chama hicho, Mwenyekiti wa Royal, Jane Mwakipunda, alisema kwa sasa chama hicho kina wanachama 20 na kwamba kinatarajia kufanya mambo makubwa ikiwamo kusaidia huduma za jamii.

Habari Kubwa