Wanawake wahamasishwa uwekezaji kwenye umeme

22Jul 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Wanawake wahamasishwa uwekezaji kwenye umeme

WANAWAKE wametakiwa kujiamini na kujitokeza kuwekeza katika sekta ya nishati ya umeme ili kuendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto, alitoa rai hiyo wakati akifungua kongamano la wanawake walio katika sekta ya nishati, lililoandaliwa na Mtandao wa Wanawake katika sekta ya Nishati Tanzania (TaWoED) na kuwakutanisha wanawake wahandisi na wanafunzi wa vyuo kwa lengo la kujadili fursa zilizopo katika sekta hiyo.
 
Kumbilamoto alisema kuwa umefika wakati kwa wanawake wenye uwezo katika uwekezaji hususani kwenye uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme kujitokeza na kufanya biashara hiyo kwa ufanisi.
 
“Nataka niwahakikishie kuwa wanawake wanaweza, na ndio maana hii leo tumeona wapo wengi waojihusisha na masuala ya uuzaji wa nishati ya umeme, kabla ya Rais hajatoa punguzo la umeme wa vijijini wa REA na mjini, sola ambayo inauzwa na kampuni za wanawake imekuwa ikisaidia jamii,” alisema na kuongeza,
 
Alisema wapo wanawake wanaotamani kupata tenda za serikali kuu au halmashauri lakini wanakutana na vikwazo lakini kwa sababu wamejitokeza itakuwa rahisi kuwapa kipaumbele.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TaWoED, Gwaliwa Mashaka, alisema wamezindua kongamano hilo kwa lengo la kuwaleta pamoja wanawake walio katika sekta ya nishati ili kuweza kujua fursa na tenda mbalimbali zinazotolewa kupitia sekta hiyo.
 
Alisema mtandao huo pia utakuwa na programu maalum kwa wanafunzi waliomaliza vyuo vikuu waliosomea masuala ya uhandisi kupata elimu na kuwafundisha kwa vitendo ili kuajirika.
 
Kwa upande wake mshauri wa masuala ya nishati kutoka Kampuni ya Geni Energy Consulting Firm, Juliana Pallangyo, aliwataka wanawake ambao wapo kwenye sekta ya nishati ya umeme kufanya kazi kwa weledi, kujiamini na kutokata tamaa.
 

Habari Kubwa