Wanawake wanufaika mikopo ya halmashauri

13Jan 2019
Dege Masoli
Handeni
Nipashe Jumapili
Wanawake wanufaika mikopo ya halmashauri

HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, imetoa mikopo isiyo na riba kwa makundi maalumu ya wajasiriamali yenye thamani ya takriban Shilingi milioni 13.6.

Mkuu wa Wilaya ya handeni Gondwin Gondwe, picha mtandao

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Vijijini, William Makufwe , aliyasema hayo kwenye mahojiano na Nipashe kuhusiana na mikakati, mafanikio na changamoto za kuwaendeleza wajasiriamali wilayani humo.

Makufwe alieleza kuwa kiasi hicho cha fedha kimetokana na kutenga asilimia 10 ya makusanyo ya halmashauri hiyo ambayo kisheria inalazimika kurejeshwa kwenye makundi hayo maalumu yakihusisha vijana, wanawake na wahitaji.

Akifafanua zaidi alisema wanafaidika kutoka makundi sita maalumu yaliyopewa mikopo kutoka kwenye asilimia 10 ya halmashauri hiyo ni vijana, kinamama na watu wenye ulemavu.

Aidha, Makufwe alitumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na maofisa wa halmashauri katika kukusanya ushuru, tozo na kodi ya serikali ili kuimarisha miundombinu na huduma nyingine za kijamii.

Aidha, Katibu Tawala wa Wilaya ya Handeni, Boniface Maiga, akizungumza na gazeti hili alitangaza vita na viongozi ngazi ya vijiji, kata na tarafa, ambao watakaobainika kujitengenezea tozo zisizo rasmi na kuchukua fedha za wananchi kinyume na sheria.

Maiga aliwataka wananchi kutoa taarifa mara moja inapotokea kiongozi yeyote anayewatoza kodi na ushuru feki ili waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Handeni, Rachel Mbelwa, katika mahojiano hayo, aliwahimiza kinamama kujiunga katika mfuko wa bima ya afya ili kupata fursa ya matibabu ya uhakika na kunusuru afya zao na za familia lakini pia kuwekeza kwenye maendeleo badala ya kutumia fedha nyingi kujitibu.

Mbelwa alieleza pia umuhimu kwa wanawake kujiunga kwenye vikundi vya uzalishaji mali na kwamba kufanya hivyo ni kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kiuchumi kwa kuweza kukopesheka.

Akitoa nasaha zake Mkuu wa Wilaya , Gondwin Gondwe, aliwatoa hofu wafanyabiashara kuhusu suala la usalama na mali zao akisema kwamba serikali imejizatiti kuhakikisha kuwa usalama unakuwepo wakati wote.

Gondwe alionya viongozi wanaotumia mwanya wa na madaraka yao kugawa maeneo ya ardhi kwa nia ya kujinufaisha na kwamba atakayelalamikiwa kuhusiana na migogoro, kashfa na changamoto za ardhi atakuwa amejihatarishia nafasi yake ya uongozi.

Pamoja na kujihatarishia wadhifa alionao hatua za kisheria pia zitachukuliwa.

Alisisitiza umuhimu wa mgawo wa asilimia 10 ya mapato kwa makundi hayo kwamba katika uongozi wake atahakikisha halmashauri hiyo inaendelea kutekeleza jukumu hilo ili makundi hayo yapate stahiki zake kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa